Kwenye moja ya series za filamu ya 'The Lion King', Simba anaonekana akiwa mnyonge, muoga anajificha kichakani; anaonekana kupoteza muelekeo baada ya kufiwa na baba yake katika umri mdogo. Rafiki ambaye ni nabii(nyani), anamjia Simba na kumwambia aache kuhuzunika kwani baba yake hajafa yupo hai, Simba anastaajabu "inawezekanaje!" Rafiki anamwambia Simba "nifuate nikakuoneshe baba yako".
Rafiki anampeleka Simba kwenye bwawa na kumwambia Simba aangalie kwenye maji atamuona baba yake, Simba anaangalia lakini anachoona ni taswira yake tu, Rafiki anamwambia Simba "angalia kwa umakini zaidi". Simba anapoangalia kwa umakini zaidi anamuona baba yake, na anamsikia akimwambia "𝑺𝒊𝒎𝒃𝒂, 𝒌𝒖𝒎𝒃𝒖𝒌𝒂 𝒘𝒆𝒘𝒆 𝒏𝒊 𝒏𝒂𝒏𝒊". Simba anapokumbuka yeye ni nani anarudi nyumbani siyo kama Simba tu bali ni 'mfalme Simba'.
Rafiki alipomwambia Simba “angalia kwa umakini zaidi”, huo ni ufunguo. Si kuangalia kwa haraka au kwa macho ya mwili tu, bali ni kuangalia kwa umakini wa roho.
Simba alipoona taswira ya baba yake ndani ya maji, hakumwona Mufasa kama aliyekufa tu — alijiona yeye mwenyewe akiwa ameendelea, akiwa na hekima, nguvu na utukufu wa baba yake. Hii inakumbusha sana mafundisho ya Yesu:
"𝑴𝒏𝒊𝒔𝒂𝒅𝒊𝒌𝒊 𝒚𝒂 𝒌𝒘𝒂𝒎𝒃𝒂 𝒎𝒊𝒎𝒊 𝒏𝒊 𝒏𝒅𝒂𝒏𝒊 𝒚𝒂 𝑩𝒂𝒃𝒂, 𝒏𝒂 𝑩𝒂𝒃𝒂 𝒚𝒖 𝒏𝒅𝒂𝒏𝒊 𝒚𝒂𝒏𝒈𝒖...;(𝒀𝒐𝒉𝒂𝒏𝒂 14:11)
Na pia:
“𝑾𝒐𝒕𝒆 𝒘𝒂𝒘𝒆 𝒏𝒂 𝒖𝒎𝒐𝒋𝒂; 𝒌𝒂𝒎𝒂 𝒘𝒆𝒘𝒆, 𝑩𝒂𝒃𝒂, 𝒖𝒍𝒊𝒗𝒚𝒐 𝒏𝒅𝒂𝒏𝒊 𝒚𝒂𝒏𝒈𝒖, 𝒏𝒂𝒎𝒊 𝒏𝒅𝒂𝒏𝒊 𝒚𝒂𝒌𝒐; 𝒉𝒂𝒐 𝒏𝒂𝒐 𝒘𝒂𝒘𝒆 𝒏𝒅𝒂𝒏𝒊 𝒚𝒆𝒕𝒖; 𝒊𝒍𝒊 𝒖𝒍𝒊𝒎𝒘𝒆𝒏𝒈𝒖 𝒖𝒑𝒂𝒕𝒆 𝒌𝒖𝒔𝒂𝒅𝒊𝒌𝒊 𝒚𝒂 𝒌𝒘𝒂𝒎𝒃𝒂 𝒘𝒆𝒘𝒆 𝒏𝒅𝒊𝒘𝒆 𝒖𝒍𝒊𝒚𝒆𝒏𝒊𝒕𝒖𝒎𝒂".(𝒀𝒐𝒉𝒂𝒏𝒂 17:21)
Umoja huu ndio siri. Sio kwamba Mungu yuko mbali na sisi, na sisi tunajaribu kumfikia. Bali Yeye yuko ndani yetu, na sisi tuko ndani yake. Tunaposahau hili, tunaishi kama Simba aliyekuwa kichakani — tunaogopa, tunajiona dhaifu. Lakini tunapokumbuka, tunasimama kama 𝐌𝐟𝐚𝐥𝐦𝐞 𝐒𝐢𝐦𝐛𝐚.
Yesu aliposema “Ufalme wa Mungu uko ndani yenu” (Luka 17:21), alikuwa anavunja dhana ya wakati ule (na hata kwetu leo) kwamba Mungu na wokovu vinapatikana mahali maalum, au baada ya kufa tu, au kupitia taratibu fulani tu. Hapana. Chanzo cha maisha yote kiko ndani yako sasa hivi.
Hivyo '𝐤𝐮𝐦𝐛𝐮𝐤𝐚 𝐰𝐞𝐰𝐞 𝐧𝐢 𝐧𝐚𝐧𝐢' si maneno ya faraja tu, ni amri ya kiroho. Ni mwito wa kurudi nyumbani ndani mwako mwenyewe, na hapo utakutana na Baba.
Na unapokumbuka wewe ni nani, unapoiona taswira ya Baba yako (Mungu) ndani yako hautakuwa mnyonge, wala mwoga, kama ilivyokuwa kwa Simba, unarudi kwa ujasiri na kusimama katika nafasi yako. Yesu alisema “Ninyi ni nuru ya ulimwengu” — si “mtakuwa nuru” au “mnapaswa kuwa nuru” — bali ninyi ni nuru. Tayari.
𝐒𝐰𝐚𝐥𝐢 𝐥𝐚 𝐤𝐮𝐭𝐚𝐟𝐚𝐤𝐚𝐫𝐢
Ni nini kinachokufanya usahau wewe ni nani mara kwa mara? Ni woga? Ni maumivu? Ni maoni ya watu? Ni dhambi au tabia fulani?
Kila mara unapohisi umepoteza mwelekeo, rudi kwenye “bwawa” — mahali pa utulivu, na uangalie kwa umakini zaidi. Utamwona Yeye. Na utasikia sauti ile ile: “𝐊𝐮𝐦𝐛𝐮𝐤𝐚 𝐰𝐞𝐰𝐞 𝐧𝐢 𝐧𝐚𝐧𝐢.”
Social Plugin