DHANA YA HOFU/WOGA KATIKA KUBORESHA MAISHA YAKO




Kutokuona kitu kilichopo ni upofu, lakini kuona kitu kisichokuwapo ni upofu mara mbili!
Woga ama hofu ni ‘hali ya kutoweza kustahimili vitisho’.
Kwa bahati mbaya sana watu tulio wengi tunaishi tukiwa katika hali ya upofu unaozidi upofu, yaani upofu mara mbili, kwamaana kwamba tunaishi tukiwa na macho ya kuona vitu visivyokuwapo; hali hii ya kuona vitu visivyokuwapo imepelekea watu wengi kutofikia malengo yetu kwakuwa mbele yetu tunaona vikwazo na vizuizi ambavyo kihalisia havipo, tunaishi kwa kutumia uzoefu wa watu wengine walioshindwa kufanikiwa katika mambo ambayo nasi tunatamani kuyafanya.
Hofu hutufanya tuone vitu visivyokuwapo. Mwanadamu hazaliwi na hofu, hofu ni hali ambayo mtu huijenga mwenyewe ama kwa kujengewa na watu wanaomzunguka na mazingira anayoishi, maandiko matakatifu yansema kuwa “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu….(2Timotheo 1:7, Warumi 8:15) ”. Hofu ina matawi makubwa matano
1. Hofu ya kushindwa
2. Hofu ya kukataliwa
3. Hofu ya kupoteza
4. Hofu ya kukosolewa
5. Hofu ya kuchekwa
Kila mtu ameumbwa na hali ya kutaka kufanya mambo fulani fulani yenye manufaa kwake binafsi, familia yake, jamii yake, nk; wengi tumeshindwa kwakuwa mbele yetu tunaona vitu visivyokuwepo, si kwamba hatuna uwezo wa kuyakamilisha mambo hayo, ila ni kwasababu tunaona na kuamini kuwa tutashindwa, tutakataliwa, tutapoteza, tutakosolewa, tutachekwa.
Amini, zaidi ya 65% ya vitu tunavyovihofu huwa havipo, si halisi. Ushauri wangu ni kuwa kiwango cha kani/nguvu unayoitumia kutengeneza mazingira ya kuona vitu visivyokuwepo, tumia kiwango hichohicho cha kani kutengeneza mazingira ya kufikia matarajio yako na hatimaye kuziishi ndoto zako.
Hofu ya kushindwa ndiyo kushindwa kwa mtu, ishinde hofu yako, boresha maisha yako, fikia matarajio yako na ishi ndoto yako.
Inuka uondoke!
Rafiki yako
Lazaro JP Kavageme.