WATOTO NDIYO NJIA NA FURSA PEKEE YA KUMFIKIA MWANADAMU NA KWELI YA MUNGU


WATOTO NDIYO NJIA NA FURSA PEKEE YA KUMFIKIA MWANADAMU NA KWELI YA MUNGU
Watoto ni matokeo, ni matokeo yenye matokeo. Watoto ni matokeo ya ushirika baina ya wazazi wawili (baba na mama), maana yake ni kuwa hakuna mtoto pasipo kuwa na ushirika wa watu wawili wa jinsia mbili tofauti.
Matokeo ni hali ama jambo linakuja baada ya kazi Fulani kufanyika. Kila kazi ina matokeo, hakuna matokeo pasipo kazi. Baada ya mitihani kufanyika huja matokeo, baada ya mashindano ya mchezo Fulani kufanyika huja matokeo, na matokeo huwa ni yaina mbili tu, 1. Matokeo mazuri, 2. Matokeo mabaya.
Matokeo mazuri huja baada kazi Fulani kufanyika vizuri, hali kadhalika matokeo mabaya huja baada ya kazi Fulani kufanyika vibaya. Kazi yeyote ikifanyika kwa kupangiliwa na mpango wenyewe kuratibiwa kwa umakini, kaz hiyo pasipo shaka italeta matokeo mazuri, na ikiwa haitafanyika vizuri na kuratibiwa vizuri, matokeo yake huwa ni mabaya
Watoto ni matokeo mazuri, kwakuwa uwepo wao ni matokeo baada ya kazi iliyonywa vizuri na kwa usahihi bila kujali mazingra ya upatikanaji wake. Watoto ni matokeo yenye matokeo, watoto kama matokeo huwa na matokeo ama mazuri ama mabaya, matokeo ya watoto ni tabia zao. Tabia za watoto hujengwa nyumbani, nyumbani ni mahali muhimu sana kwa makuzi ya watoto.
Kwakuwa wazazi ndiyo viongozi wa nyumba, wao wanahusika pasipo shaka juu ya makuzi ya watoto wao kwa asilimia 90, na asilimia zingine 10 hugawanywa kwenye mazingira nje na nyumbani, yaani shuleni, mtaani, ndugu jamaa na marafiki nk.
Watoto huzaliwa pasipo tabia, wanakuwa ni sawa sawa na kitabu kisichoandikwa kitu ndani yake; mtoto hujengewa tabia siku kwa siku kadri anavyokuwa, na wajenzi wa tabia ya mtoto ni wazazi, walezi mmoja mmoja, na mfumo wa maisha ya hapo nyumbani; tabia ya mtoto hujengwa na kuwa tabia kama matokeo ya jambo fulani kutendwa kwa kurudiwa rudiwa, kama ilivyo kwenye matokeo, na tabia nazo zipo mara mbili, yaani tabia mbaya na tabia nzuri, tabia hizi mbili zinayo makundi tabia mengi na tofauti tofauti, mfano, kukata tama, kupenda kujisomea, uongo, wizi, maombi, uchonganishi, upatanishi, kusamehe, kujitolea, kujifunza, ukarimu, nk.
Utoto ni hatua ya kwanza ya maisha ya mwanadamu katika kukua, hatua ya pili ni ujana, tatu ni ut uzima, na nne ni uzee. Piramidi ya idadi ya watu nchini Tanzania inaonesha kuwa idadi kuwa ya watu nchini Tanzania ni watoto wenye umri chini ya miaka 15 na vijana; kwa hiyo ukicheza na tabia za watoto unacheza na tabia za watu wa taifa husika. Hakuna mtu anapenda kuwa mtu mwenye tabia mbaya, tusipowalea watoto wetu na kuwahudumia katika njia ifaayo basi tutakuwa tunajitengenezea taifa la watu wa hovyo hovyo.
Kwa maana hiyo, ni muhimu watoto wahudumiwe, kuhudumia mtoto kuna maana pana zaidi, inahusu uangalizi na ufuatiliaji wa karibu wa mtoto, ulinzi, makuzi yake, kutimiza mahitaji yake ya lazima ya siku kwa siku kama chakula na maji salama, mavazi, makazi, elimu bora, afya, habari, hadi atakapokuwa mtu mzima. Huu ni wajibu wa kila mtu kwenye familia, dini, jamii, na taifa.
KWANINI TUWAHUDUMIE WATOTO:
1. Moyo wa Mungu kwa Watoto:-
Aya mbalimbali katika Biblia zinaonesha namna Mungu anavyowachukulia Watoto kipekee katika Moyo wake; tazama simulizi ya kisa kile katika ile familia takatifu { Ibrahim, Sara, Isaka; Hajiri, na Ishmaeli}. Mwanzo 21.
Katika mazingira hayo Mungu alisikia kilio cha Ishmaeli, ‘ Mungu akasikia kilio cha kijana’ mwanzo 21:17.
Hajiri wa kale anawakilisha wanawake wengi katika historia na hasa wengi wa nyakati zetu, wengi wanapewa mimba na kuachwa wakihangaika na watoto peke yao, wametelekezwa, kutengwa, na kuachanizwa. Wengine wameachwa wajane katika umri mdogo tu na wale ndugu wa marehemu waume zao wanawanyang’anya mali zote; wajane hawa wanabaki hawana kitu na wakati huo huo wana watoto wa kuwasomesha na kuwatunza. Katika mazingira kama haya kina mama wengi wanatafuta njia za kuwanusuru watoto wao bila mafanikio, wanapoteza matumaini na wanaishia kuwatelekeza watoto pia.
Hajiri ni kivuli cha Kanisa na jamii ya Kikristo. Kuna mambo kadhaa ya kujifunza kutokana na hatua anazochukua Hajiri kuhusiana na hali ya Ishmael. Ni kwa kiasi gani Kanisa na jamii vinaona na kushiriki maumivu ya Watoto walio katika mazingira magumu; kanisa na jamii vinatii maagizo kuhusu kuwahudumia Watoto?, kuwatia moyo, na kuwawezesha kuvuka katika mazingira hatarishi kwa maisha yao na utu wao wote kwa ujumla? {Mungu alimwagiza Hajiri aondoke kwenda kumwinua Ishmaeli na si Ishmaeli kumwinua Hajiri}.
Kuhusu kujitenga kwa Hajiri:-
Kanisa na jamii wapo umbali gani kutoka Watoto walipo? Kanisa halijawatenga Watoto Kitheologia, kilitulgia, ama kimafundisho? Kuna vipaumbele gani katika mipango ya Kanisa juu ya Watoto?
Ni nani anafundisha Watoto Kanisani, {waaalimu wa Sunday school na kipaimara}.
-umri wao, ni wazee sana ama ni vijana?
-vipi kuhusu elimu zao, wanawafahamu Watoto Kisaikolojia, Kijamii, na
Kiimani.
-Watoto wakihudhuria ibada za wakubwa wanapewa nafasi gani?
Ishmaeli anawakilisha Watoto wengi katika ulimwengu wa leo wale walioachwa katika maumivu na hatari ya kuharibika na hata kufa. Watoto wengi wanaishi bila ya kuwa na uhakika wa kupata chakula cha uhakika na kufaa wakati wote, hawana uhakika wa matibabu wanapougua, hawapati elimu, na hawana faraja. Watoto wengi wameachwa katika uangalizi wa House girls na Television. Watoto wengi wameachwa na kutengwa na siasa za nchi, na familia, na wakati mwingine hata Kanisa limewatenga Watoto. Wengi wa Watoto hawa wapo mitaani wakipambana na hali za kimazingira onevu{baridi kali, njaa, kiu, jua kali, mvua na madawa ya kulevya}; hakuna ajuaye mwisho wao utakuwaje. Ishmaeli ni sauti ya Watoto aliaye kwa uchungu wa kuachwa, kutengwa, na kunyanyaswa na jamii pamoja na mazingira.
Simulizi hii inaonesha na kudhihirisha Moyo wa Mungu kwa Ishmaeli, siku zote Mungu husikia kilio cha Watoto, anawaona walipolala, huwapelekea msaada, anawatuma wajumbe, anabaini mpango, na anaagiza tuwaendee. Moyo wa Mungu huugua juu ya Watoto katika mazingira magumu waishimo na katika njia ngumu wapitiazo. Agizo la Mungu kwetu ni kuondoka na kwenda kwa Watoto kuwainua na kuwashika mikononi mwetu.
Biblia inazo aya nyingine zinazobainisha Moyo wa Mungu kwa Watoto; macho yake yanawaona kabla hawajakamilika{Zaburi 139:13-16}, anawachunga tangu wakingali wadogo {Zaburi 22:9-11, Zaburi 68:5,6}, na anataka wao waaminio wawatunze watoto yatima {Yakobo 1:27,}, anawabariki na kuwatunza watoto {Kumb 1:39}, anaagiza watu wazima wawatunze na kuwafundisha watoto {Mithali 20:7, Zaburi 103:13, Waefeso 6:2, Wakolosai 3:21}, na anakasirishwa na yeyote anayewanyanyasa watoto {Walawi 18:21, Kutoka 22:21-23, Zaburi 72:4, Mathayo 18:6}, Mungu anaagiza tuomboleze kwa ajili wa watoto {Maombolezo 2:19}. Nk.
2. Mungu anaagiza Watoto wahudumiwe:-
Kuhudumu ni ile namna ya kuwa karibu na yeye anayehudumiwa, yaani kumsikiliza kwa upendo, kushiriki mawazo na hisia zake, kufurahi naye wakati wa kufurahi, kulia naye, na kuzitafsiri fikra zake za ndani katika mwili wa nje: Ni kuthamini, kujifananisha naye kwa kushuka naye akishuka {unyenyekevu}, na kujitofautisha naye kwa kumpa heshima ya juu zaidi yako. Lakini pia kwa kumwelekeza na kumchagulia jambo jema la kutenda, na kuisimamia imani.
Zile fikra za kwamba Watoto wapewe uhuru wa kuchagua imani wanayotakiwa kuifuata watapokuwa na uwezo wa kuchagua, fikra hizi si sahihi tena. Namna ya kuwahudumia Watoto ni kazi nyeti sana kwa maana “Watoto ndio njia”, ukiwaelekeza vibaya watakuwa wabaya hasa, ama vinginevyo, “ mtoto mleavyo ndivyo akuavyo”. Unyeti wenyewe unakuja kwa kuzingatia kwamba Watoto wanapatikana katika taasisi nne tofauti katika makuzi yao kiimani, kisaikolojia, na kijamii; {a}nyumbani, {b}shuleni, {c}kanisani, ama dini nyingine, {d}kwa ndugu, jamaa na marafiki..
Ipo namna ya kuwahudumia Watoto kiimani, kisaikologia, na kijamii; hasa ikizingatiwa kuwa Watoto wapo katika makundi rika manne japo matatu ndio muhimu zaidi kuyazingatia hapa, ya miaka miaka 3-6, miaka 7-11, na miaka 12-18: kila kikundi hapa kinayo mahitaji yake kiimani, kisaikolojia, na kijamii, kila kimoja tofauti na kingine. Lakini izingatiwe kuwa pia malezi kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki huwa ni tofauti na yale ya kinyumbani, hivyo zipo athali kubwa {mbaya ama nzuri} kwa makuzi ya Watoto zinapotokea tofauti za kimalezi, hali kadhalika shuleni hasa kwa wale wanaowapeleka Watoto kusoma mbali na nyumbani.

3. Yesu Kristo aliwapa Watoto kipaumbele:-
Katika jumla nzima ya utendaji wa Yesu, yako maeneo manne ya ushhuhuda wa Yesu kuwa na vipaumbele vyake kwa Watoto:-
-Aliwakaribisha kwake, walipokuja kwake ili awawekee mikono yake juu yao. Mathayo19:13-15, Mk 10:13-16, Lk 18:15-17: Katika kisa hiki,
wanafunzi wa Yesu walitaka kuwazuia Watoto wasimkaribie Bwana, yeye anapoliona jambo hilo Hakupendezwa nalo. Yesu alisimamisha yote aliyokuwa akiyafanya ili kuwahudumia Watoto kwanza. Pengine wanafunzi wa Yesu hawakuwa na nia ya kuwazuia kabisa labda walitaka wawaruhusu waje kwa Bwana atakapokuwa amemaliza shughuli zake kwa siku hiyo, lakini kinyume nao Yesu aliwataka Watoto waje kwanza.

-aliitakabari na kuithamini ibada ya sifa ya Watoto. Wakati wa Jumapili ya Mitende, siku Yesu alipoingia Yerusalemu kwa shangwe, na siku Yesu alipolitakasa Hekalu.
Mathayo 21ff. katika kisa hiki, Watoto walipanda madhabahuni na kupaza sauti za shangwe wakimshangilia Bwana “Hosana mwana wa Daudi”, alipokuwa akizipindua meza za wabadili fedha, na kuwafukuza wote waliokuwamo hekaluni kwa biashara.
Angalia! Wakuu wa Makuhani walikasirishwa sana na kile kitendo cha Watoto kupanda madhabahuni. Yesu aliithamini sifa na ibada ya Watoto Mathayo 21:16.

-Aliwashirikisha Watoto katika Huduma yake. Yesu alipowalisha watu maelfu nyikani, alichagua kutumia chakula {samaki na mikate} cha mtoto ili kutenda muhujiza huo. Yamkini walikuwepo watu wazima karibu waliokuwa na chakula pia, Yesu hakuwachagua hao. Yohana 6:1-14.
-alitumia Mtoto kama kielelezo {si mfano} cha halitabia ya ufalme wa Mungu. Ili kuweza kuingia mbinguni haina budi mtu kuwa kama Mtoto mdogo. Lakini pia Yohana aliona kuwa Watoto ni sehemu ya kanisa 1Yohana 2.
4. Ibilisi anataka kuwaangamiza Watoto:-
Simulizi nyigi katika Biblia juu ya ukatili waliotendewa Watoto zipo ili tujue kuwa, hata Setani anajua kuwa Watoto ndio njia na fursa ya kipekee ya kumfikia mwanadamu na kweli ya Mungu; kwa namna Mungu anavyowekeza katika Watoto ili kuleta hali bora katika maisha yao na hata kuifikia mbingu,
na Ibilisi naye anawekeza kwa Watoto ili kuupinga mpango mwema wa Mungu kuhusu Watoto. Kwa namna Mungu anavyotumia watu wake kufanikisha lengo, hata shetani anao watu wake ili kuupinga mpango mwema wa Mungu. Mfano wa Farao, Herode Mkuu, na lile Joka kuu.
-Farao aliagiza Watoto wakiume wa Waebrania wote wanaume wauawe {waliokuwa wanazaliwa} lengo ni ili taifa la Mungu lisikue na kusitawi. Kutoka 1:8-22.
-Herode Mkuu aliagiza Watoto wote wakiume wa umri wa miaka 0-2 katika Bethrehemu wote wauawe. Lengo ni ili kumuua Yesu Mfalme wa Wayahudi. Mathayo 12:16
-Joka kuu, linawakilisha namna zote za kishirikina, matambiko, mila na destuli zisizofaa kwa wana wa Mungu. Uf 1:13-17.
Hata sasa Ibilisi bado anataka kuuwa Watoto, zipo kumbukumbu nyingi zioneshazo namna anavyowatesa, kuwanyanyasa, na hatimae kuwaua kabisa Watoto, angalia vita visivyokoma katika maeneo mengi katika dunia ya tatu, na utoaji mimba; wapo watoto walioshikishwa bunduki na kupangwa katika safu za mbele vitani, wapo waliodhalilishwa utu wao kwa kubakwa na kufanyishwa kazi ngumu kwa muda mefu pasipokuwa na muda mzuri wa kupumzika. Kwa maelfu wameuawa vitani, kwa maelfu wamekufa kutokana na madhara ya vita vyenyewe, na kwa maelfu wamebakia walemavu, na yatima wasiokuwa na makazi.
5. Upo uwezekano wa kuinuka kizazi kingine:-
Tangu baada ya kutoka Misri utumwani taifa la Mungu Israel halikuwahi kuingizwa tena katika mateso, fitina, na unyanyaswaji kutoka kwa jamii nyingine yeyote; isipokuwa hadi wakati wa Waamuzi baada ya kuingia Kanaani nchi ya ahadi, na hii ilitokea hasa baada ya kifo cha Yoshua.
Mwandishi wa kitabu cha Waamuzi anajumuisha mtindo wa maisha walioishi na kanuni za maisha walizozifuata taifa la Israel, tangu Kumbukumbu la Torati la Musa hadi Yoshua, na baada ya hapo mtindo wa maisha ulibadilika. Waamuzi 2:8-23.
Ni dhahiri kwamba muendelezo wa taifa lolote unategemea kudumishwa siyo tu kwa maadili mema lakini hasa muendelezo wa imani sahihi katika Mungu kwa njia ya kufundisha Watoto. Watoto wasiporithishwa imani sahihi kwa njia ya mafundisho ya msingi na maisha ya imani kwa ujumla. Pasipo shaka yeyote baada ya kizazi kiaminicho kuondoka, kitakuja nyuma kizazi kingine kisichomjua Mungu. Iwapo Watoto hawatahudumiwa kwa dhati, siku zinakuja na roho ya kizazi kingine itasambaa na kutenda kazi katika familia zetu, katika nchi yetu Tanazania, na hatimaye katika Ulimwengu wote.

Watoto ndio njia, Watoto ndio fursa, Watoto ndio udongo mzuri.
Kwenye mfano wa Mpanzi, Mathayo 13:1-9, Lk 8:4-15; Zipo awamu kuu nne za maisha ya mwanadamu kiumri kulingana na aina nne za udongo katika mfano huo.
  • Awamu ya kwanza; ni umri zaidi ya miaka 60, kwa kawaida watu katika umri huu wanao uelewa mpana sana kimaisha kutokana na kuwa wamekutana na mambo mengi sana ya kupanda na kushuka, kusitawi na kuporomoka, ama kuendelea mbele na kurudi nyuma, wameishashiriki siasa na hata biashara, kusafiri huko na kule na kufanya kazi mbalimbali na katika mazingira tofauti tofauti, wameishatumika kanisani na nje ya kanisa, wanaelewa taratibu nyingi za kanisa, kanuni na taratibu zote za kanisa, wameisha wasikia wahubiri na waalimu wengi wakihubiri na kufundisha: Katika jumla nzima ya maisha yao upo uzoefu wa kutosha kimaisha kiasi cha kuwafanya kuwa sugu. Katika umri huu watu huwa hawapendi kujaribu kufanya jambo jipya, maana yote wanayajua, mara nyingi hukaa viti vya nyuma kabisa kanisani “ ni watu wa matambiko na mapokeo” yaani hutekeleza jambo bila kuulewa msingi wake ama kuzingatia maana ya jambo lenyewe.
Awamu hii ya maisha ya mwanadamu inalandana na mbegu ambazo zilianguka katika udongo ambao chini kulikuwa na mwamba. Ni rahisi zaidi kumfikia mwanadamu na ujumbe kamili wa Mungu, na kumfanya kuwa mwanafunzi wa Yesu kabla hajaufikia umri huu, vinginevyo itakuwa ni lazima kushughulika na mwamba {uzoefu wa maisha na dini}.
  • Awamu ya pili; ni ya umri kati ya miaka 45-60, katika umri huu watu hukutana na changamoto mbalimbali tena za kipekee sana, kama kusomesha na malezi ya familia kwa ujumla, kusimamia na kuratibu miradi mbalimbali ili kujikimu kimaisha, kazi nyingi, na kujiandaa na maisha ya kustaafu; katika awamu hii watu wapo katikati ya shughuli na mambo mengi yenye tija ama yasiyokuwa na tija kwa jamii na kanisa. Awamu hii imelandana na udongo wenye miiba inayoisonga kweli ya Mungu. Ili kuwafikia watu katika umri huu inabidi kupambana na miiba kwanza.
  • Awamu ya tatu; ni ya umri kati ya 20-35, katika umri huu wengi wao ni vijana wenye misisimko na kutaka kujionesha. Hushiriki katika matukio mengi na mikutano ya kiroho, hupenda kuimba na kushangilia zaidi ya
kusikiliza na kutafakari neno. Vijana katika umri huu wanakutana na vishawishi vingi vyenye kuwapotosha, migahawa ya internet, vipindi fulani vya televisheni na sinema zisizofaa, majumba ya muziki, utumiaji wa madawa ya kulevya, magazeti na majarida yasiyofaa, na falsafa za utandawazi {hawa ni ndege}. Katika awamu hii, vijana wanafikika, ila inabidi kupambana na ndege kwanza.
  • Awamu ya nne; ni Watoto chini ya miaka 20, katika awamu hii upo urahisi wa kumfikia mwanadamu, tafiti zinaonesha kuwa asilimi 80 ya watu wanaookolewa na kudumu katika wokovu ni wale wanaookoka wakiwa na umri wa miaka 4-14. hivyo yafaa kupanda kwa Watoto kwa umakini na kwa usahihi, kupanda kweli ya Mungu katika ujumla wake mtimilifu, awamu hii inalandana na udongo mzuri.
Kumbe kazi ya kumfikia mwanadamu na kumleta katika utimlifu wa Mungu ni ngumu kadri mtu anavyoongezeka umri, kuna kupambana na ndege, kupambana na miiba, na tukichelewa zaidi kuna kupambana na mwamba.
Kwa wengi wetu Watoto wanadhaniwa kwamba hawana mchango wowote wa maana katika familia, kanisa na katika jamii. Maandalizi ya kushiriki kikamilifu baadae ni matokeo tu ya kushiriki kikamilifu wakingali Watoto wadogo. Sikuzote Watoto ni sehemu hai ya familia, kanisa, jumuiya, na taifa. “kwahiyo Huduma ya Kanisa si kamilifu bila Huduma kwa Watoto”. Familia, kanisa, jumuiya, na taifa vinapaswa kuifanya Huduma ya Mtoto kuwa ni sehemu muhimu kwa uhai na utendaji wake na kiini katika yote wayafanyayo. Ipo haja ya kuwahudumia Watoto ili kuwawezesha na kuishi sasawa na mpango wa Mungu kwa maisha yao.
Hudumia mtoto/watoto, hudumia taifa lako!
Watoto ni thawabu toka kwa Bwana,
Watoto ni mishale mikononi mwa Shujaa,
Watoto ni kama miche ya Mizeituni,
Watoto ni kama nguzo katika nyumba ya Mungu,
{Zaburi 127:3-5, 128:3, 144:12, Malaki 4:6}
Rafiki yako,
Lazaro JP Kavageme