SHABAHA 10 ZA ELIMU.
1. Iwe ni ile ya kujenga barabara za kiwango cha lami zinazounganisha mioyo ya watu.
2. Iwe ni ya kujenga hospitali zinazoleta jawabu la matibabu ya kansa ya ubaguzi na madonda ndugu yotokanayo na kutokusameheana katikati ya watu wa jamii zetu.
3. Iwe ni ya kujenga viwanja bora vya ndege na bandari zinazoleta na kubeba abiria wanaosafiri kusambaza upendo.
4. Iwe ni ya kujenga madarasa yanayokutanisha watu wanaotafakari kupata majawabu ya maswali magumu ya hatima ya jamii zetu kimila na kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi.
5. Iwe ni ya kujenga vyuo vya ufundi vinavyotoa mafundi wa kupatanisha ndugu wanaokosana na kukataa suluhu katika jamii zetu.
6. Iwe ni ya kujenga viwanja wanapokutana washindani wanaoshindana kwa hoja na kukubaliana ama kutokukubaliana kwa hoja kwenye majadiliano yanayohusu maslahi mapana kijamii.
7. Iwe ni ya kujenga nyumba bora juu ya viwanja vilivyopimwa wanamokaa watu wanaolijua kusudi la kuishi kwao na wanaoziishi ndoto zao.
8. Iwe ni ya kujenga reli ya standard gauge itakayopitisha kwa kasi elimu ya upendo, uvumilivu, kiasi, na subira miongoni mwa wanajamii.
9. Iwe ni ya kujenga mabomba yanayopitisha maji safi na salama wakati wote ili kusafisha umbumbumbu unaotamalaki katika jamii zetu wa kutegemea njia za mkato na uchawi kupata utajiri.
10. Iwe ni ya kujenga miundombinu ya umeme wa uhakika kufika kila kaya na kijiji kuleta nuru katika fikra za watu.
Ikiwa elimu tunayoipata/tuliyoipata shuleni/chuoni, hailengi hata shabaha moja wapo kati ya hizi, basi elimu hiyo haina tofauti na nguvu za giza, ambazo hulenga kuwatia watu hofu.
Ikiwa sisi tunaojiita wasomi katika kizazi hiki hatulengi yeyote kati ya shabaha hizo, basi sisi ni washirikina wazamivu, sisi ni wachawi wabobevu, ni walozi waandamizi serikalini na kwenye mashirika, sie ni wanga tu; vyeti vyetu si mali kitu, yafaa vifungiwe vitumbua na pemba.
Tafakuri jadidi!
Social Plugin