KANUNI 12 ZA UONGOZI



Kila mtu ni kiongozi. Kozi hii ni kwaajili ya watu wote yaani viongozi wa familia (baba na mama)vikundi, viongozi kazini, na wafanyabiashara.
Dhana ya uongozi ni kuonyesha njia, kuifuata njia, kumjenga na kumlinda kila anayeifuata njia hiyo.   
Tafsiri ya maneno kutoka dhana ya uongozi:-             
A.   Kuonyesha njia: Ni kuweka wazi namna ya kufika kule watu wanapopaswa kufika, ni wajibu wa kiongozi kuwaonyesha njia wale anaowangoza kuifuata
B.   Kuifuata njia: Kiongozi akiisha kuwaonyesha njia wale anaowaongoza yafaa yeye awe wa kwanza katika kuifuata njia hiyo.
C.   Kumjenga mtu ni kumpatia mafundisho yanayotakiwa kuhusu njia anayoifuata ili aweze kuitembea kwa uhuru na ujasiri.
D.   Kumlinda mtu, ni kumhakikishia usalama wake na mali zake huyu unayemuongoza. Ndivyo mungu alivyofanya kwa Israeli alipowatoa Misri, Nehemia 9:19 hata hivyo wewe kwa wingi wa rehema zako hukuwaacha jangwani; nguzo ya wingu haikuwaondokea wakati wa mchana, ili kuwaongoza njiani; wala nguzo ya moto haikuondoka wakati wa usiku, ili kuwapa mwanga na kuwaonyesha njia watakayoiendea.


1.    Dhihirisha tabia za Mungu: Kila mtu ameumbwa kwa mfano wa Mungu, kwahiyo tunazo baadhi ya tabia za Mungu, Wakolosai 3:12-13 Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu,mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.

2.    Tunza na heshimu familia: Mungu ndiye mwanzilishi wa familia, baada ya kumuumba mwanadamu wa kwanza Adamu na Hawa aliwapa na maelekezo ya namna kuwa na familia.. Kila kitu huanzia nyumbani, huduma, biashara, ufundi nk. 1Timotheo 5:8 Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini. Kwahiyo familia ni kitu cha muhimu sana mbele za Mungu, usiiache familia yako nyuma ya kazi, biashara, ama huduma, daima familia inaanza ndipo vingine vyote vinafuata. Heshimu pia familia za wenzako.

3.    Dumisha moyo wa ibada: Kiongozi mzuri ni yule anayemuhusisha Mungu kwenye kila jambo lake, asili ya hekima ni Mungu, kwa hivyo ni muhimu sana kuwa karibu naye wakati wote. Manabii waliomba, hata Yesu alikuwa na tabia ya kuomba. Lakini pia ni muhimu kwa kiongozi kuwa na ushirika na watu wengine kwaajili ya ibada. Waebrania 10:25 wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.

4.    Uadilifu: Tafsiri ya neno uadilifu ni kutenda sawa sawa na makubaliano, au kama tulivyokubaliana. Ni muhimu sana kwa kiongozi kusimamia makubaliano, nje na kusimamia makubaliano migongano lazima itatokea. Waefeso 4:1 Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa;

5.    Tumikia: Kiongozi mzuri ni yule mwenye kutanguliza kutumikia na sio kutumikiwa, yaani kiongozi mtumishi wa watu, kwa mfano wa Yesu. Marko 10:45 Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi. Hivi ndivyo Bwana Yesu alivyofanya, hakuwa akitumikiwa bali alitumikia wengine.

6.    Sikiliza: Kusikiliza hapa inamaanisha kutenda ama kufanya kama unavyoshauriwa na wenzako, kiongozi mzuri husikiliza wenzake. Ni muhimu sana kuwasikiliza wenzako maana unapokuwa kiongozi haimaanishi kwamba wewe una akili zaidi ya wenzako. Usipowasikiliza wenzako utakuwa unajijengea ukuta baina yako na wenzako, na hivyo utajikuta unakuwa na mzigo mzito mno kuubeba peke yako. Mithali 1:5 mwenye hekima asikie na kuongezewa elimu, na mwenye ufahamu ayafikie mashauri yenye njia.

7.    Ujasiri: Kuwa jasiri haimaanishi hakuna vitu vya kuogopesha, jasiri ni yule anayetekeleza wajibu wake pasipo kuogopa vitisho anavyokutana navyo.Joshua 1:9 Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako. 2Timotheo 1:7 Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.

8.    Chochea moto wa huduma: Kwakuwa kiongozi ni yule anayewatangulia wenzake, basi haimstahili yeye kuwa mlegevu na msinziaji. Kiongozi hapashwi kulala kabla matokeo hayapatikana. Tunawezaje kuuchochea moto ulio ndani yetu; ni kwa kuomba, kusoma neno, kujifunza (hudhuria semina), na kuendelea kufanya jambo kulingana na wito wako. Yeremia 20:9 Nami nikisema, Sitamtaja, wala sitasema tena kwa jina lake; basi, ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia.

9.    Dumisha mawasiliano sahihi: Kiongozi mzuri ni yule anayewasiliana na wenzake kwa kutumia lugha inayoeleweka kwao. 1Wakorintho 14:8 Kwa maana baragumu ikitoa sauti isiyojulikana, ni nani atakayejifanya tayari kwa vita?

10. Wajengee uwezo wale unaofanya nao kazi: Usitake kuvuna matunda kwenye mti ambao haukuumwagilizia, kujenga uwezo wa mtu ni kumuwezesha, kumpatia maarifa sahihi ili aweze kufanya shughuli uliyompangia kufanya. Waefeso:4:12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; Muhubiri 10:10 Iwapo chuma hakipati, wala mtu hakinoi; Ndipo hana budi kutumia nguvu zaidi.

11. Tenda kwa ubora wakati wote: kiongozi mzuri ni yule anayetafuta kuwa bora yeye mwenyewe kwanza ndipo ahimize ubora kwa anaowaongoza. Hapa kuna kujiendeleza ili kupata maarifa mapya, kiongozi ni mtu wa kujiendeleza/kujifunza kila siku. Wakolosai 3:23 Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu,. Unapofanya kazi kwa ubora wajuu sana pasipokujali kazi hiyo ni ya muda mfupi, ama ni kazi ambayo haukoisomea hata hivyo, pasipokujali unalipwa kidogo sana, jua kwamba unajijengea mazingira ya kupata fursa nzuri zaidi kwenye maisha yako. Luka 16:10 Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia.

12. Weka kumbukumbu: Kiongozi mzuri ni yule anayeandika kumbukumbu za mambo muhimu kuhusu familia, kazi, huduma, na biashara. Unapoandika inakusaidia kujikumbusha baadae. Nehemia 7:6 nakuendelea, Hawa ndio wana wa wilaya, waliokwea kutoka katika ule uhamisho wa hao waliokuwa wamechukuliwa, ambao Nebukadreza, mfalme wa Babeli ,aliwachukua mateka,nao wakarudiYerusalemu na Yuda,kila mtu mjini kwake.ndio hawa waliokuja pamoja na Zerubabeli, Yoshua, Nehemia, Seraya, Reelaya, Nahamani, Mordekai, Bilshani, Mispari, Bigwai, Rehumu, na Baana. Hii ndiyo hesabu ya wanaume wa watu wa Israeli; Wana wa Paroshi, elfu mbili mia moja sabini na wawili.Wana wa Shefatia, mia tatu sabini na wawili. Wana wa Ara mia sita hamsini na wawili…… Ufunuo 2:1 Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu.