Unakijua kile kilichomo ndani yako?



Kila kitu kinachoonekana nje ya mtu, kama matendo yake, maneno, na muonekano wake, ni matokeo ya kile kilichomo ndani yake. Namna mtu anavyojichukulia ni matokeo ya hali yake ya ndani, yaani fikra zake ama mtazamo wake; kimtokacho mtu ndicho kiujazacho moyo wake; mtu alivyo ni matokeo ya fikra zake; watalam wa afya pia husema kuwa mtu alivyo ni matokeo ya chakula anachokula, maana yake ni kuwa nuru ya mwili ama uhafifu wa mwili wa mtu ni matokeo ya chakula anachokula. Kila kitu huanzia ndani. Kilichomo ndani ya mtu huathiri maisha yake.

Hakuna jambo ama kitu akifanyacho mtu pasipo kuliwaza kwanza bila kujali amewaza kwa muda mrefu ama ndani ya muda mfupi, kila kitu kinaanzia mawazoni. Mchoraji huchora kitu ambacho tawira yake imo mawazoni mwake, hata wasanifu majengo hali kadhalika; mchoro uliowazi katika karatasi ni mchoro ulio wazi katika fikra za mchoraji. Mwandishi yeyote kabla ya kuweka kalamu yake kwenye karatasi nakuanza kuandika habari fulani, habari hiyo huwa ipo tayari katika fikra zake.

Hakuna ubaya ama uzuri wa mtu unaoonekana isipokuwa ulianzia ndani. Hii inaathiri maisha yetu ya kila siku na mahusiano yetu kwenye jamii, mfano mtu anapokuwa muuguzi, mwanasheria, mwalimu, na kazi nyingine nyingi, pamoja na biashara fulani na kilimo; ili mtu afanye kazi hizi kwa furaha na bashasha ni lazima ana msukumo kutoka ndani yake. Daima mtu hukifanya kwa furaha kile kitokacho ndani yake, kinachoonekana nje ni tafsiri ya kilicho ndani, ukiona mtu anafanya kitu asichokifurahia kama ni kazi, biashara nk, jua kuwa kitu hicho hakitoki ndani yake, anafanya kwa shinikizo, na katika mazingira haya si rahisi kabisa mtu kufanikiwa katika hicho anachokifanya.

Nukuu"ikiwa kuamka kwako asubuhi na kwenda kazini ni kwasababu unatakiwa kufanya hivyo basi tambua ya kuwa wewe ni mtumwa wa hicho ukifanyacho, na nafasi ya kufanikiwa kwako ni ndogo sana; lakini kama unaamka asubuhi na kwenda kazini kwasababu unataka mwenyewe basi wewe ni mtawala na mtu huru, nafasi/uwezekano wa kufanikiwa katika hicho ukifanyacho ni kubwa na ipo wazi mbele zako".

Kila mtu ana kitu ndani yake ambacho kinaweza kumsaidia kuleta mabadiliko makubwa kwenye maisha yake. Mwandishi maarufu Steve Siebold, katika kitabu chake The 77 mental toughness effects of the world class, anasema “watu hununua kitu kilichomo ndani ya muuzaji kwanza kabla ya kununua kile anachokiuza”, anamaanisha kuwa watu/wateja humfuata mtu/muuzaji kutokana na namna anavyowahudumia.

Kila kitu huanzia ndani. Unakijua kilichomo ndani yako? Unaijua nguvu ya hicho kitu? Unakitumiaje?

Rafiki yako, Lazaro JP Kavageme