UPENYO NI NJIA

                  images

Mazingira yanayomzungukwa mwanadamu mara nyingi huwa si mazingira rahisi kwake, hayafanyi njia rahisi kwake katika kuyafikia matarajio yake na kutimiza ndoto zake; tangu shuleni mwanadamu anakutana na mazingira ambayo hayampi urahisi wa kutimiza ndoto zake, kwenye biashara, kazi nk.

Ipo jitihada ambayo ni lazima mwanadamu aitumie na ni lazima apitie mchakato fulani hivi ili kuyafikia matarajio yake, mchakato huu huwa mara nyingi huwa si rahisi. Mchakato ulio rahisi ninaufaninsha na njia pana, na usio rahisi ninaiita upenyo.

Upenyo waweza kuwa ni ufa, sehemu nyembamba ama tundu, ni mahala ambapo si rasmi kwa matumizi yeyote yale ya mwanadamu

Maumbile ya asili yanamuongoza mwanadamu kupita katika njia/barabara na si hewani, njia ni mahala sahihi kwa mwanadamu kupita kuelekea mahali anapokusudia kufika, ni tofauti na upenyo, si rahisi mtu akatumia upenyo kama njia, watu hutumia upenyo kupita pale inapowalazimu sana. Lakini ikiwa mwanadamu anaweza kupita katika upenyo kuifikia matarajio yake, maana yake upenyo unakuwa ni njia, upenyo ni njia.

Watu wengi duniani wamepata kufanikiwa baada ya kupita kwenye mpenyo. Matajiri wengi, wajasiriamali wakubwa, wanamichezo maarufu, viongozi wengi wa kisiasa, wanamuziki, wacheza filamu, waandishi, nk, wamepata kutimiza ndoto zao kwa kupenya, kupita kwenye upenyo, kwa kujitengenezea njia.

Ukiwa unapita njiani na ghafla ukakuta njia hiyo inafika mwisho wake lakini si mwisho wako, kwa maana ya kuwa haujafika kule unakokwenda, tafuta upenyo, daima huwa kuna upenyo, kuwa kama maji yanayokwenda, yanapofika mahali penye njia yake pakawa na kikwazo huwa ni lazima yatafute upenyo ili kuendelea na safari.

Usijali madhara unayoweza kuyapata ama kusababisha katika mchakato wa kupenya, daima tazama ndoto/matarajio yako; usiridhike na safari inayoishia mahala njia inapoishia; tengeneza njia.

 

Upenyo ni njia.

 

Rafiki yako,

Lazaro JP Kavageme