TAFUTA KUJUA NINI MAPENZI YA MUNGU JUU YA NAFASI YA UONGOZI ULIYONAYO

 




2Wafalme 21:1-18, 22.

Katika kusoma kitabu cha pili cha Wafalme sura ya 21 kuna simulizi ya mfalme Manase aliyeitawala Yuda (Ufalme wa Kusini) vibaya, huyu hakuwa mfalme mzuri, alifanya mambo ya hovyo sana na kulikosesha taifa la Yuda kiasi Mungu aliazimia kuleta mabaya juu ya watu wa ufalme wa Yuda. Kwenye sura ya 22 simulizi inaendelea na hapa tunamkuta mfalme Yosia ambaye ni mwijukuu wa mfalme Manase na mrithi wa kiti cha ufalme wa Yuda, maandiko yanamtaja mfalme Yosia kuwa ni mfalme mzuri aliyemcha Mungu sana; mfalme Yosia aliamua kuyatafuta mapenzi ya Mungu juu ya Ufalme wake, katika kumtafuat Mungu huku Yosia anapata kujua ya kwamba kuna ghadhabu ya Mungu iliyokuwa imeachiliwa wakati wa mfalme Manase babu yake ambyo wakati wa utimilifu wake ulikuwa umewadia, baada ya kujua hili mfalme Yosia anaamua kujinyenyekeza mbele za Mungu na Kuomba rehema za Mungu ili aipishie mbali ghadahbu ile. Maandiko yanaeleza kwamba Mungu alisikiliza sauti ya kilio cha Yosia na akaiahirisha ghadhabu ile isije juu ya Yuda wakati wa mfalme Yosia.

Kutokana na mistari hii tunajifunza kwamba ni muhimu sana kutafuta kuyajua mapenzi ya Mungu juu ya nafasi yako kiuongozi mahali popote, iwe ni kazini kwako, kwenye biashara yako nk; hata kwenye familia tafuta kuyajua mapenzi ya Mungu juu ya ubaba wako au umama wako. Katika kutafuta tafuta huko lipo jambo Bwana atakufunulia ambalo litakuthibitisha juu ya wajibu wako kama baba na kama mama. Yawezekana unakaa katika eneo/kiti ambacho kina ubaya ambao katika huo Mungu ana kisasi nacho, yawezekana watangulizi/mtangulizi wako kwa kujua ama kwa kutokujua alimkosea Mungu kiasi cha kumuudhi sana, sasa ili kujua kama kuna kisasi cha Mungu ama hakipo tafuta kujua nini mapenzi ya Mungu juu ya kiti chako na eneo lako.

Kwenye familia yawezekana kujua ama kwa kutokujua mababa waliingia maagano na ufalme wa giza kama alivyofanya mfalme Manase, yawezekana sana magano yale yanatenda kazi hadi leo na yanaathiri familia, biashara, na kazi yako. Ni katika kutafuta kujua nini mapenzi ya Mungu tutafunuliwa kujua asili ya ubaya wote unaotuandama.

Tenga muda wa kusoma Neno, kuomba, kusikiliza maelekezo ya Mungu juu ya jambo lako.

Barikiwa.