NI NANI ANAMMEGEA MWENZAKE MKATE?


“Kumegeana mkate si kwa chakula tu, bali ni maisha yote ya taabu, furaha, na maisha yote kimwili na kiroho”

Imani ni maisha ambayo ili yawe na maana kwetu ni lazima tuyatafakari na kuyajadili kwa pamoja. Ni lazima kuelimishana na kupeana mwanga, tusiamini kama Watoto wachanga bali tuamini kama watu wazima wenye kuwajibika.

Imani ya Kikristo ina matukio makubwa mawili, {a}kuzaliwa, na {b}kufa na kufufuka kwa Kristo.  Siku chache zimepita tangu tulipoadhimisha kufa na kufufuka kwake Kristo zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita.

“Alipoketi kula chakula pamoja nao, alichukua mkate akabariki, akaumega, akawapa. Na macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua; lakini yeye akatoweka kati yao” Luka 24:30-31.

Luka katika sura ya 24:13-35 anaeleza kisa cha kushangaza kidogo baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kisa kinatokea k atika barabara ya kwenda Emau. Labda hii ni barabara ya kiimani, maana hata Mtume Paulo, anakutana  na Kristo na kuwa mfuasi wake wa kweli katika barabara hii.

Katika barabara hiyo, Kristo aliwatokea Wafuasi wawili, cha kushangaza ni kuwa ndugu hawa wawili hawakuweza kumtambua japo walitembea naye na kuongea naye kwa muda juu ya matukio mbalimbali ya Yerusalemu, na hasa tukio la kifo cha Kristo. Wakati wote huo waliokuwa wakizungumza naye bado hawakuweza kumtambua, upo ushahidi kuwa hata baada ya ufufuo bado Kristo alibaki katika sura ileile, hakubadilika. Tazama maandiko katika luka 24:38-39, na Yohana 20:27.

Kutokana na ushuhuda toka katika maandiko hayo, ni kweli kuwa Kristo alifufuka na mwili wake. Lakini wale Wanafunzi wa Emau hawakuweza kumtambua. Inashangaza! Ila walipomkaribisha ndani kwao wakati wa chakula, alimega mkate akaanza kuwagawia, kwa tendo hilo wakamtambua, kwa nini iwe hivyo?

Jibu pekee la kuondoa mashaka yote ni kwamba kitendo cha kumegeana mikate, kitendo cha kukumbuka wengine kwanza, kitendo cha kugawa chakula kwa wengine kwanza, kilifanywa na Kristo peke yake. Hiki ndicho kitambulisho chake kikubwa. Vinginevyo hakuna, hakuna maelezo ya wafuasi wake walioishinaye, wakasafiri naye na kusikiliza mahubiri yake, wamsahau na kumkumbuka tu alipoumega mkate na kuwagawia wao kwanza.

Jamii ya wakati wa Yesu na jamii yetu leo ni kuwa, mtu anakula kwanza kabla ya kuwakumbuka wengine, ni kwamba mikono inaelekea kinywani kwanza kabla ya kuwagawia wengine. Kila mtu anashughulikia uhai wake kwanza, kila mtu anatafuta mali zake kwanza, kila mtu anashiba kwanza, ndiyo maana wengine wanakula na kusaza na wengine wanalala na kufa kwa njaa!

Uhakika wa hili kwanza tunaupata pale Kristo alipofanya muujiza wa kuongeza mikate na samaki. Mitume walikuwa na chakula chao, walitaka wale chakula chao, na wale waumini wengine waende kutafuta chakula chao huko mjini: “Basi Yesu aliwaita wanafunzi wake akasema, ‘nawaonea watu hawa huruma kwasababu kwa siku tatu wamekuwa nami, wala hawana chakula. Sipendi kuwaacha waende bila kula wasije wakazimia njiani’, wanafunzi wakamwambia, ‘hapa tuko nyikani, tutapata wapi chakula cha kuwatosha watu wengi hivi? Yesu akawauliza “mnayo mikate mingapi?” wakamjibu, “saba na samaki wachache”. Basi Yesu akaamuru watu waketi chini. Akaichukua ile makate saba na wale samaki, akamshukuru Mungu, akavimega, akawapa wanafunzi nao wakawagawia watu wote wakala, wakashiba…” Mathayo 15:32-37.

Saba ni namba takatifu, haina maana kwamba walikuwa na mikate saba. Kwa maneno mengine mitume walitaka kusema walikuwa na mikate ya kuwatosha wao tuna si ule umati wa watu, lakini Yesu alitaka umati ule kwanza kabla ya mitume na yeye.

Hapa ndipo ujumbe na upekee wa Kristo Yesu umelala; yaani kuwakumbuka wengine kabla yako wewe! Na mkate unayachukua maisha yote. Mkate ni chakula, na chakula kinaleta uzima. Hivyo kumegeana mkate ni kumegeana uzima!

Matatizo ya dunia yetu yamelala hapa. Ni kwamba katika hali ya kawaida, hali ambayo haina imani ya Kimungu, kila mtu anajiangalia yeye kwanza, ashibe yeye kwanza, kila familia inajiangalia kwanza, kila taifa linajiangalia kwanza kabla ya kuangalia usalama wa taifa jingine kwanza. Umaskini, vita, na taabu zote za dunia yetu ni kwamba hatutaki kumegeana mkate!

Baada ya kufundisha kwa muda wa miaka mitatu, Yesu aliwaaaga mitume kwa fundisho ambalo linabeba ujumbe wake hapa duniani: “halafu akatwa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema: “huu ndiyo mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka” Luka 22:19.

Walipoandika injili hawatuambii kuwa Yesu alikula kwanza. Tunachosoma ni kuwa alimega mkate  na kuwapatia kwanza. Na akawaambia kwamba wakitaka kumkumbuka na kukumbuka mafundisho yake, wamegeane mikate!

Hata jumuiya nyingi za Kikristo zilitambuliwa kwa kitendo cha kumegeana mikate. Hivyo na wafuasi wake wale wa Emau walimtambua tu kwa kumega mkate, hawakumtambua kwa sura yake, sauti yake au kitu kingine.

Kila mwaka tunaposheherekea Sikukuu ya Pasaka, tunakumbwa na mafumbo ya kufa na kufufuka na fumbo la msalaba na kuuchukua kama ishara yetu kubwa. Tunakumbwa na utamaduni wa kufanya sherehe hii kila mwaka, ila hatuzami katika tafakuri ya ujumbe wa Kristo ya kumegeana mikate.

Ni nani anammegea jirani yake mkate? Katika Kanisa, katika Ushirika, katika mitaa, vipi katika familia?

MBONA MSALABA WAKO UMENAKSHIWA NA KUWEKWA DHAHABU?

Msalaba umekuwa ishara kubwa ya Kanisa. Viongozi wengi wa dini {Wakristo} wanavaa mikufu yenye misalaba shingoni kama ishara ya Ukristo au kumwakilisha Kristo ndani na nje ya Kanisa. Makanisa yanajitambulisha kwa ishara ya msalaba, hata Wakristo walio wengi wanajitambulisha kwa kufanya ishara ya msalaba kwa kila tendo jema wanalotaka kulifanya ama shukrani.

Msalaba umetolewa kwenye hali yake ya kubeba majuto na mateso na badala yake umenakshiwa na kupambwa kwa dhahabu! Msalaba haukuwa wa dhahabu, haukunakshiwa, ulikuwa mti tu.

Yote haya yanatendeka ama kimaksudi ama kwa kutokujua kuwa ishara ya Wakristo sio msalaba bali ni kumegeana mikate. Lakini hata kama ni lazima sana kutumia msalaba basi sio wa dhahabu!