Ushindi wa mwanadamu dhidi ya dhambi hausababishwi na mzingira aliyopo. Mafanikio yeyote katika kitu chochote (biashara, kazi, nk) hayategemei mazingira, hali ya hewa, nk. Shetani alimshinda Adam na Eva wakiwa bustanini Edeni tena wakiwa wameshiba nyama pori na matunda (balanced diet) lakini akamshindwa Yesu akiwa jangwani kwenye ukame. Unaweza kuwa umezungukwa na vile vitu ambavyo watu wanadhani hauna sababu ya kushindwa na ukashindwa. Unaweza kuwa na vyeti vizuri sana vya shule, na ukashindwa na wale wasio navyo, unaweza kuwa na wazazi wazuri sana na ukashindwa na wale wasiokuwa nao. Na vingine ongezea wewe.
Bustani ya Edeni ni kielelezo cha utajiri, utukufu, ukuu, baraka. Jangwa ni kielelezo cha ufukara, mashaka, utasa.
Pointi kubwa hapa ni kwamba mazingira uliyokulia ama uliyopo bila kujali ni Edeni ama ni Jangwani, hayana uhusiano wa moja kwa moja na hali yako ya sasa, iwe ni kiuchumi au kiroho.
Katika hali ya kiuchumi kuna mataifa yapo jangwani na ni mataifa tajiri sana kuzidi yale yaliyo kwenye ardhi ya maji mengi, ardhi yenye rutuba, na mvua za kutosha. Nchi kama Dubai, Saudi Arabia, Israel, Misri nk, ni majangwa matupu lakini ni tajiri kuliko nchi nyingi za dunia ya tatu ambazo zina mito, maziwa, bahari, na ardhi yenye rutuba.
Kilichotofautisha kati ya Adam na mrembo wake Eva ni nguvu za roho, neno linasema Yesu alipanda jangwani akiwa amejazwa nguvu za roho na akaongozwa na Roho Mt. Adamu na mrembo wake waliongozwa na mwili wakakwama.
Nguvu za roho ni nini. Ni ufahamu wote kuhusu Mungu na nafasi ya mwanadamu katika Ufalme wa Mungu. Ile mwanzoni Mungu anapoanza kuumba ulimwengu, neno linasema "Roho wa Mungu akatulia juu ya uso wa maji, Mungu akasema na iwe nuru". Nuru aliyoiumba Mungu kwenye siku ya kwanza haikuwa jua, mwezi, wala nyota, hivi vyote viliumbwa siku nyingine, siku ya nne. Sasa nuru hii ni ipi, ni nini? Nuru huu ni ule uwezo, maarifa ya kutafsiri mazingira na kuyaamuru yaitikie utashi wako. Maarifa haya, nuru hii ndiyo ile roho iliyomuongoza Yesu jangwani. Yesu anaingia jangwa akiwa na maarifa ya kutosha kuhusu mazingira na wito wake, hivyo aliyafanya mazingira yatii utashi wake ambao ndiyo kiini cha wito wake duniani.
Usichanganye kunena kwa lugha, kuomba kwa muda mrefu, kutoa mapepo, na nguvu za roho. Hii ni kijisehemu tu katika uwezo wa Roho Mtakatifu. Kama nina haya yote halafu sifanikiwi katika maeneo mengine ina faida gani?
Katika somo hili Yesu anasema nitachipusha ushindi katikati ya jangwa lako, kama alivyoshinda yeye na wewe utashinda. Chochote kile unachopitia chenye sifa za ujangwa, kutengwa na wana familia, kudharauliwa, majuto, utasa, kiburi cha watoto, kiburi cha unaowaongoza, hasara kwenye biashara, hasara kazini, madeni, hofu zote, mashaka yote. Yesu anasema utashinda katika yeye.
Tumuombe Yesu atusaidie kuamsha ile nuru ya mwanzo. Atujaze maarifa, ufahamu na nguvu ya Roho ili jangwa letu liitikie wito wetu. Atufanye washindi katika Yeye. Amen🙏
𝙒𝙖𝙛𝙞𝙡𝙞𝙥𝙞 4:13
𝙉𝙖𝙮𝙖𝙬𝙚𝙯𝙖 𝙈𝙖𝙢𝙗𝙤 𝙔𝙤𝙩𝙚 𝙆𝙖𝙩𝙞𝙠𝙖 𝙔𝙚𝙮𝙚 𝘼𝙣𝙞𝙩𝙞𝙖𝙮𝙚 𝙉𝙜𝙪𝙫𝙪.
Social Plugin