Heri Yako

Kutokupata unachotaka kunaweza kuwa baraka. 

Hapo zamani palikuwa na Sultan mmoja ambaye alichagua mzee mmoja rafiki yake kuwa Msaidizi wake mkuu. Sultan na Msaidizi wake walikuwa pia wanawinda wanyama porini pamoja mara kwa mara. Baada ya muda, wananchi wakaanza kulalamika kwa Sultan kwamba Msaidizi wake huyo hana msaada
wowote kwa watu, kwamba kila anayeenda kumuelezea shida yake yeye huwa anajibu "Heri Yako". 

Sultan akasikitika lakini akamvumilia. Sasa ikatokea siku moja Sultan akapata ajali ya kudondoka kutoka kwenye farasi wake na kukatika kidole. Yule Msaidizi alipopata taarifa hizo za Sultan kukatika kidole akasema: "Heri Yake". Sultan alivyoambiwa maneno ya Msaidizi wake akakasirika akaamuru akamatwe, awekwe ndani. 

Ikafika siku Sultan akataka kwenda kuwinda. Kwa kuwa Msaidizi/rafiki yake kamuweka ndani, akalazimika kwenda kuwinda mwenyewe. Akawinda kutwa nzima, baadaye akaanza kuchoka. Kwa mbali akaona hema, akasema ngoja nikawasalimie waliomo na kupumzika kidogo. Kumbe wenye hema ile ni majangili/wahalifu wa msituni. Walipomuona tu wakasema "tumewinda siku tatu bila mafanikio, tulikuwa tunatafuta mtu wa kutoa kafara, tunashukuru umejileta". Wakati wanajiandaa kumchinja, mkubwa wa majangili akaamuru wamkague mwili mzima kwanza. Wakakuta kidole kimoja kimekatika. Mkubwa wao akasema masharti ya kafara ni lazima isiwe na kasoro ya kimaumbile. Sultan akapona. Akarejea mbio kwenye mji wake. 

Akakumbuka maneno ya Msaidizi wake (Heri Yake). Akaamuru atolewe. Akamuomba msamaha kwa kumweka ndani. Mshauri akamjibu kwamba "uliponiweka ndani nami nilijisemea Heri Yangu. Manake ningekuwa nje tungeenda wote kuwinda na kwakuwa mimi sina kasoro ya kimaumbile, mimi ndio ningetolewa kafara". Wakakumbatiana.

Kama una masikitiko na maumivu makubwa kuhusu jambo ulilolitaka sana lakini ukalikosa, HERI YAKO. Kwenye kukosa unachotaka pia kuna heri zake.

Mshukuru Mungu tu.