CHANJO


Katika ulimwengu wa tiba watu huchanjwa kwa ajili ya kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali, kama vile kifua kikuu, surua, ugonjwa wa kupooza, na ndui. Katika kupewa chanjo kwa ajili ya kinga dhidi ya ugonjwa fulani, kwa mfano, kifua kikuu, mtu huwekewa vijidudu vya ugonjwa huo anaochanjwa dhidi yake. Kwa kifua kikuu mtu huwekewa vijidudu au bakteria wanaosababisha kifua kikuu. Lakini, vijidudu anavyowekewa mtu kwa ajili ya chanjo huwa na sifa kuu mbili. Kwanza, huwa havina nguvu ya kutosha kusababisha ugonjwa huo ndani ya mtu aliyechanjwa navyo. Pili, huwa vina tabia na uwezo wa kupambana na kuvishinda vijidudu vya ugonjwa huu vinapoingia mwilini, ambavyo kama visingeshindwa vingesababisha mtu kupata huo ugonjwa. Kwa hiyo mtu huyo ana kinga na kwa hiyo hatapata ugonjwa huo. 

Katika nadharia ya mawasiliano, utafiti umebaini kwamba mtu akipewa ujumbe ambao una ukweli kidogo na hafifu kuhusu jambo fulani, atakapokutana na ukweli kamili wa jambo hilo, ukweli kidogo na hafifu aliotangulia kujua utamfanya akatae ukweli kamili kwa kuzalisha hoja za kutosha kupinga au kukataa ukweli kamili. Hivyo, ukweli kidogo na hafifu hufanya kazi ndani ya mtu mithili ya kinga ya chanjo.

Hii ina maana kwamba watoto wakipewa mafundisho hafifu ya mambo ya imani, hata kama ni sahihi na kweli, lakini siyo kamili, mafundisho hayo hayatawawezesha kuamini na kubadilika lakini watoto watakapokutana na maelezo kamili ya ukweli hafifu waliotangulia kuupokea kana kwamba ndiyo kweli yote watapinga au kukataa ukweli kamili. Wanakuwa wamechanjwa dhidi ya kweli kamili, na kwa hiyo wamezuiliwa wasiujue ukweli. 

Kijana tajiri ambaye habari zake zimeandikwa katika Marko 10:17-21 (pia Mathayo 19:17-21) ni mfano wa kijana aliyekuwa amechanjwa dhidi ya kweli kamili. Kijana huyu alikuwa amefundishwa amri kumi na kuzishika tangu utoto wake, yaani akazielewa na kuzitekeleza. Hata hivyo,
bado alikuwa na swali la msingi kwamba ingempasa afanye nini ili ajihakikishie kwamba ataurithi uzima milele. Yesu alipomtaka awe radhi kuacha vyote (kukariri torati na udini)na badala yake ashike na kuelewa mafundisho ya Yesu Kristo, kijana yule alishindwa kupokea msaada aliouhitaji, kutoka kwenye chanzo chake halisi – Yesu - na badala yake akaondoka amekasirika. Alikuwa amefundishwa dini na amri na alikuwa amelelewa kwenye utamaduni na ustaraabu wote wa dini. Vitu hivyo, pamoja na uzuri na umuhimu wake, havikufanya moyo wake ubadilike, maana havikuwa kweli kamili: lakini pia vilisimama kama kinga ndani yake vikamfanya ashindwe kupokea kweli kamili kutoka kwake aliye Kweli yote. Alikuwa amechanjwa kiasi hicho, na kwa hivyo alikuwa amezuiliwa asije kwa Yesu (hakujua kwamba kuelewa mafundisho ya Yesu kungelimpa mwanga kuielewa vizuri zaidi torati na dini yake). Yafaa izingatiwe hapa kwamba kisa cha kijana huyu tajiri kinafuata mara tu baada ya kisa cha Yesu Kristo kukasirishwa na kitendo cha wanafunzi wake kuzuia watoto wadogo wasije kusikiliza mafundisho yake. 

Watoto ndiyo njia na fursa pekee ya kumfikia mwanadamu na kweli kamili. Wapo watoto kiumri na wapo watoto kiimani, nadharia nk. Hawa wa pili ni wakubwa kiumri lakini ni watoto katika imani ama nadharia fulani. Hawa wote wasipopewa mafundisho kamili ya jambo, mafundisho na ukweli huo nusu hufanyika kuwa chanjo dhidi ya ukweli kamili.

LKavageme
Inuka Tuondoke Ministries 
Mwanza - TZ