MBUZI ALIYEPOTEA

Kisa hiki kilianza Jumapili moja alasiri katika mji mdogo huku Usukumani.

Marafiki wawili wanafunzi walikuwa na wazo la kuwawezesha kukwepa adhabu ya siku iliyokuwa ikiwakabili kutoka kwa waalimu  sababu ya utukutu wao shuleni.

Siku hiyo walishauriana kukusanya mbuzi watatu kutoka zizi la babu jirani na kuchora namba 1, 2 na 4 ubavuni mwa kila mbuzi.

Usiku huo waliwaachia mbuzi ndani ya jengo la shule yao.

Asubuhi iliyofuata, waalimu walipoingia shuleni, walisikia harufu mbaya.

Punde waliona kinyesi na mikojo ya mbuzi kwenye ngazi na karibu na mlango wa kuingilia na kugundua kuwa mbuzi walikuwa wameingia ndani ya jengo hilo.

Msako ulianzishwa mara moja na punde si punde, mbuzi hao watatu walipatikana.

Lakini waalimu walikuwa na wasiwasi, mbuzi namba 3 alikuwa wapi? Walitumia kutwa nzima kutafuta mbuzi namba 3.

Hatua kwa hatua kulikuwa na hofu na kuchanganyikiwa waalimu na wanafunzi.

Mkuu wa shule alitangaza kuahirisha masomo kwa wanafunzi kwa siku nzima kwakuwa Walimu, walinzi, wafanyakazi wa canteen, na wavulana wote walikuwa na shughuli nyingi wakitafuta mbuzi namba 3, ambae kwakweli na bila shaka, hakupatikana kamwe kwa sababu tu hakuwepo. 

Maisha daima yanatupa kuhisi 'ukosefu wa ukamilifu/utimilifu' kwenye mambo mengi sana, kazini, kwenye mahusiano, kwenye biashara, tunajihisi kutokamilika, kutotimia, kutotosha; na sote kwa namna moja ama nyingine tunaacha vyote na kujipa kazi ya kutafuta mbuzi namba 3, ambaye kwakweli hata hayupo. 

Mungu alipomuita Gideoni kazini, Gideoni hakujiona kutosha, anamwambia Mungu kuwa yeye anatoka katika ukoo maskini sana na yeye ni kitinda mimba kwenye familia yake. Waamuzi 6:15. Nabii Yeremia anapoitwa kazini hakujiona kutimia anamwambia Mungu "siwezi kusema; maana mimi ni mtoto". Yeremia 1:6

Kutokuwepo kwa kitu siku zote ni kukubwa kuliko uwepo wa vitu vingine vingi. Hali hii imeua ndoto za watu wengi.