Jua wito wako, itika.

Mfalme Sauli na Daudi
Kisa kutoka kitabu cha 1Samweli sura ya 18 kuanzia mstari wa 9 hadi sura ya 31.

Kwenye simulizi ya mfalme Sauli, Daudi ndiye msifiwa japo si simulizi yake. Kwenye simulizi ya Daudi, Daudi ndiye msifiwa japo mfalme Sauli yupo. Chuki ya mfalme Sauli juu ya Daudi ndiyo inayomuinua zaidi Daudi kiasi cha kuwa msifika kwenye simulizi isiyo yake. Daudi aliujua wito wake na aliitika, mfalme Sauli aliujua wito wake lakini hakuitika. Chuki, husda, na wivu wa mfalme Sauli juu ya Daudi havikumsaidia Sauli bali vilimsaidia sana Daudi. Bidii ya mfalme Sauli kutaka kumuua Daudi haikumfanya mfalme Sauli kuwa shujaa bali kulimfanya Daudi kuwa shujaa na maarufu kwenye simulizi isiyo yake.

Kushindwa kwa mfalme Sauli vitani dhidi ya Wafilisti ilikuwa ni matokeo ya ukosefu wa maandalizi ya hakika ya vita, wakati mfalme Sauli yupo bize kumshughulikia Daudi, Wafilisti walikua bize kujiandaa na vita kumshughulikia mfalme Sauli. Wakati ulipowadia, Wafilisti wamejiandaa kwa vita wakati mfalme Sauli hajajiandaa kwa vita. Ilikua ni vita ya kustukiza kwa mfalme Sauli, matokeo yake akapoteza uhai na ufalme.

Somo: Jua wito wako, itika, ili kwenye simulizi yako tujifunze zaidi kuhusu wewe na si mtu mwingine; kuujua wito wako pasipo kuitika unatoa nafasi ya mtu mwengine kuonekana zaidi kwenye simulizi yako kuliko wewe mwenye simulizi; Usipoitikia wito wako kila vita juu yako itakua ni ya kustukiza; Na, jiweke mbali na wivu, chuki, na husda dhidi ya mtu, vitu hivi vitatu hualika watu wengine kuwa nyota kwenye simulizi yako; unapokuwa na wivu, chuki na husda juu ya mtu fulani, jua kuwa umempa mtu huyo utawala wa maisha yako.

Ukiujua wito wako na kuitika, umeepuka chuki, wivu, na husda dhidi ya watu wengine.