Kuwa na kiasi katika kunena

Mithali 6:2 
Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako,

Kwenye Kanuni 48 za Mamlaka, kanuni ya 4 inasema "kuwa na kiasi katika kunena" {Always say less than necessary} 

Mwaka 1825, Kondraty Reyleyev alihukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kuhamasisha migomo yenye lengo la kuishinikiza serikali ya Urusi kufanya mabadiliko kadha wa kadha kwenye sera ya viwanda ya taifa hilo. Siku ya kunyongwa ikawadia, kwa nasibu kamba ya kunyongea ikakatika Reyleyev akiwa ameshaning'inia. Kwa desturi tukio kama hili lilipotokea mtu alipaswa kusamehewa. Akiwa analijua hili Reyleyev kwa kejeli akasema "si mnaona, katika Urusi hakuna jambo linafanyika sawasawa, hata kutengeneza kamba imara tumeshindwa". Habari ya kukatika kamba ikamfikia Nicolous I aliyekua kiongozi (Czar) wa Urusi wakati ule, na mara moja akaanza kusaini hati ya msamaha kwaajili ya Reyleyev, baada ya kusaini akamuuliza tarishi "Reyleyev amesema neno lolote kutokana na tukio hilo?" Yule tarishi akamweleza Nicolaus Imaneno aliyoyasema Reyleyev. Nicolaus akasema "sawa, basi tutathibitisha", akachana ile hati ya msamaha na kuamuru hukumu ya kunyongwa Reyleyev irudiwe, safari hii kamba haikukatika.

Wahenga walinena "Mdomo uliponza kichwa". 

Mara ya mwisho kucheki ni nini kinakukwamisha ilikuwa lini na uligundua nini?

Wakati huu cheki mdomo wako, huenda ndiyo unaokukwamisha.