Nuru yang'aa gizani

Yohana 1:5 Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza.

Usilolijua hautolijua hadi utake kulijua. Giza halifukuzi nuru bali nuru hufukuza giza; giza halina gharama bali huja kwa gharama ya kukosa nuru. Aonaye gizani ana nuru naye asiyeona nuruni ana giza machoni.

Aliye gizani asipoitafuta nuru kama si kwa hisani ya mwenye nuru kumpelekea nuru, basi yeye huyu hubaki gizani.

Muumba hakuumba giza, giza ni matokeo ya nuru isiyokuwepo, na hapo hakuna amri kuzuia nuru isije gizani, "ikawa nuru ikawa giza".

Giza lisichoondolewa huwa na tabia kuunda tumbo, tumbo la giza ni kiza totoro. Utotoro wa giza huua uhuru wa nafsi, pasina uhuru wa nafsi huzaliwa utumwa.

Muumba hakuumba utumwa, utumwa ni matokeo ya uhuru wa nafsi uliofishwa, nafsi kufishwa ni matokeo ya giza lisichoondolewa kilipounda tumbo.

Muumba alimuumba mtu huru wa nafsi si mfungwa na kumpa utashi kwamba ama aishi nuruni ama gizani, mtu huyu huchagua mwenyewe baina ya hizo mbili chaguzi.

Giza hakina gharama kuja, bali huja kwa gharama ya nuru isiyokuwapo. Daima maisha yaenda, tuwapo nuruni ama tuwapo gizani.

Daima maisha yaenda.