KIONGOZI WETU NI MUHIMU AKAWA SHOCK ABSOBER (shokomzoba, shokapu)


Mathayo 20:26

Neno shock ni neno la lugha ya kiingereza linalomaanisha mtikisiko; neno absober pia ni neno la lugha ya kiingereza linatokana na kitenzi absorb yaani kufyonza, kunyonya, haiishii kunyonya tu bali na kukifanya hicho kilichonyonywa kuwa sehemu yake (shock absober) na kukigeuza kifae kisiwe na madhara tena. Neno hili limetoholewa kutoka Kiingereza na kuwa shokapu kwa Kiswahili.

Shokapu ni kifaa muhimu sana kwenye mfumo mneso (suspension system) wa gari. Kifaa hiki unaweza kukidharau unapokitazama kinapokuwa nje ya eneo lake maalum. Kazi kubwa ya shokapu ni kumeza/kuzuia mitikisiko inayotokana na gari kupita kwenye njia mbovu isimfikie abiria aliye ndani ya gari. Na kisha huigeuza hiyo mitikisiko iwe mineso ya gari, sasa mineso hiyo ndiyo inayompa abiria kujisikia vizuri (unyado) awapo safarini, hiyo ni kazi ya shokapu. Shokapu zinapoharibika raha ya kuendesha wala kupanda gari inakwisha kabisa, na zisipokuwepo ndiyo kabisaa haifai. 

Wataalam wanasema, shokapu husaidia gari kusimama kwa wakati mara tu breki zinapotumika, shokapu mbovu huchelewesha gari kusimama kwa umbali wa mita 2 baada ya breki kutumika. Kwamaana hiyo ni rahisi sana kwa gari yenye shokapu chakavu kusababisha ajali, ama itazingonga gari nyingine kwa nyuma, ama itatumbukia mtaroni.

Gari lisilo na shokapu, ama lenye shokapu chakavu ni sawa sawa na kwama ama toroli, hauwezi kuwa na furaha ya safari ikiwa chombo cha usafiri wako ni kwama kwenye njia mbovu.

Maisha yetu ya kila siku ni sawa sawa na gari inayotembea kwenye njia mbovu, yenye makorongo, mawe, madimbwi, na vitu vingine vingi ambavyo huifanya safari ya maisha yetu kutokuwa na utulivu. Pamoja na kwamba tunapitia njia mbovu hivyo, lakini bado si lazima sana tukawa kwenye mitikisiko hiyo kiasi cha kuichukia safari yetu kabisa.

Mingi ya mitikisiko iliopo kwenye familia na kwenye jamii zetu ipo kwasababu viongozi wamepungukiwa ama wamepoteza kabisa uwezo wa kumeza mitikisiko. Kiongozi anapokosa kutimiza wajibu wake kama shokapu tazamia safari yenye mazongezonge.

Kiongozi anayetufaa ni yule mwenye tabia ya shokapu, mwenye kufyonza mikitisiko na kuigeuza kuwa mineso. 

Kiongozi asipohimili na kumeza mitikisiko mahali alipo, kila kitu kitatikisika na kuumia. Uongozi ni kumeza mitikisiko kwa usalama wa familia na taifa.