Kusudi la maisha na mahusiano ya watu wengine


Zaburi 60:7-8  Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu, Na Efraimu ni nguvu ya kichwa changu. Yuda ni fimbo yangu ya kifalme,
8 Moabu ni bakuli langu la kunawia. Nitamtupia Edomu kiatu changu, Na kumpigia Filisti kelele za vita.

Mahusiano baina ya mtu na mtu, familia na familia, kampuni na kampuni, huduma na huduma, taifa na taifa, hutumbukia nyongo pale tunapowaweka watu kwenye nafasi zisizo zao kulingana na walichobeba yaani kusudi la kuishi kwao kiuwiano na wakati uliopo.

Kwenye mistari hiyo hapo juu, Mungu anaeleza wasifu wa makabila ya Israeli ambayo ni Manase, Efraimu na Yuda, kisha anaeleza kuhusu uhusiano alionao na mataifa ya Moabu, Edomu, na Wafilisti, kwamba wasifu huo ndiyo unaoamua uhusiano wake Mungu na makabila na mataifa hayo, kwamba uhusiano alionao umejengwa juu ya msingi wa kusudi la uwepo wa kila kabila na kila taifa.

Bakuli la kunawia haliwekewi mboga. Bakuli la kunawia halipewi nafasi penye baraza la mashauri (Efraimu), bakuli la kunawia halipewi kazi ya hukumu (Yuda).

Mungu anatufundisha kwamba ili kuishi kusudi ni lazima mtu awe na mahusiano na watu wengine wenye muelekeo sawa sawa na kusudi lake, ni vigumu mtu kuliishi kusudi ikiwa hatakuwa na watu sahihi yaani watu wenye muelekeo sawasawa na wa kwake kulingana na wakati;

Kumvalisha silaha za vita Moabu ambaye ni bakuli la kunawia akusaidie kupigana na Filisti wako ni kujikosea na utapoteza hiyo vita. Kumchukulia Filisti kama Moabu ambaye ni bakuli la kunawia utakuwa umealika adui karibu yako zaidi.

Kumchukua Efraimu na kumuweka mahali pa Yuda ni kujikosesha, na kumchukua Yuda na Efraimu kuwaweka mahali pa Gileadi na Manase ni kujikosesha.

Naifaninisha hii na timu ya mpira uwanjani, kila mchezaji huwa na nafsi yake uwanjani na ile nafasi ya mchezaji uwanjani huwa imeamuliwa na kusudi la kuwepo kwake kwenye timu, kumchezesha mchezaji mbali na nafasi yake ni kumkosea mchezaji na timu nzima.

Sasa kujua nani wa kumuweka karibu nawe na huyo nani akae karibu yako wakati gani ni muhimu sana maana si kila nani anafaa kuwa karibu yako wakati wote. Kujua ni nani wa kufanya naye vita na wakati gani wa kufanya vita ni muhimu sana, maana si kila wakati utafanya vita na kila mtu.

Barikiwa!