![]() |
Mama pamoja na Mtoto wake |
Zipo sababu nyingi zinazoweza kupelekea watoto wa kike kupata mimba za utotoni wakiwa nyumbani, hapa ninataka kujadili sababu moja tu kati ya nyingi unazozifahamu.
Sababu moja wapo ya wasichana kupata mimba za utotoni ni "upendo na uhuru" uliokosekana nyumbani. Mtoto hajawahi kusikia akiambiwa "nakupenda mwanangu" pengine hajawahi kumsikia baba ama mama akimwambia mwenzake "ninakupenda". Kila mtu anahitaji kupendwa na kuoneshwa upendo hadharani na sirini. Kwa bahati mbaya sana watoto wengi wanakua wakijua kuwa baba/mama ni mtu wa kuelekeza, kuonya, kukaripia, na kusahihisha tu, kwahiyo kinachokuwapo kwenye ufahamu wa mtoto ni kusahihishwa, kuonywa, na kukaripiwa kwa kila anachokifanya; kusahihishwa/kurekebishwa na kuonywa si jambo baya hapa inahusika pia sauti (tone) inayotumika na sura anayoivaa mzazi anapokuwa akimsahihisha ama kumuonya mtoto; sauti inapokuwa ya juu yenye ukali na sura ngumu tegemea anayeonywa na kusahihishwa lazima atajenga hofu na kutojiamini; busara ni kuonya kwa upole kama maandiko matakatifu yanavyohimiza. Katika mazingira ya namna hii sasa mtoto anapopata nafasi kukutana na mtu anayeonesha kujali hisia zake, kuheshimu mawazo yake na kumpenda kwa vitendo na kumtamkia kwa maneno iwe sirini ama hadharani, hapo ndipo tatizo linapotokea.
NYUMBA KAMA MAHABUSU: Watoto wengi baada ya kupata watu wanaoonesha kuwapenda na kuheshimu mawazo yao, hujiona kuwa huru na wenye furaha, kwahivyo hupenda zaidi kuwa nje na nyumbani zaidi ya kuwa nyumbani, maana nyumbani si mahala wanapopafurahia labda kama wazazi hawapo. Watoto wengi huwa hawawamisi wazazi wao wanapokuwa nje na nyumbani na hasa wanapokuwa safarini na wanatamani wake huko kwa muda mrefu maana kwao hiki ni kipindi cha kuwa huru angalau ni kipindi kifupi, wakati huu watoto huwa na furaha zaidi kuliko wazazi wanapokuwepo. Familia za namna hii ni aghalabu sana/mara chache sana kukuta watoto na wazazi wapo pamoja sebuleni wakizungumza na kujadiliana mambo fulani fulani pamoja wakifurahiana na kucheka, mara nyingi ukikuta wapo pamoja ni ama kuna kesi, ama watoto wana mahitaji fulani kutoka kwa wazazi wao, ama ni kipindi cha sala/ibada, na baada ya hapo hakuna mazungumzo ya ziada ni kutawanyika, utasikia watoto wakichekea chumbani ama nje ya nyumba maana mbele ya wazazi hawana hata hamu ya kucheka.
UTII BILA UHURU NI UTUMWA: Kwa kujua ama kutojua madhara yake wazazi wengi wanafurahia hali hii ya watoto kuwa watiifu bila uhuru. Wanachofurahia wao ni kuona watoto wanatekeleza maelekezo na maonyo yao pasipo mjadala, wanafurahia kuona watoto wanawaogopa kiasi cha kuwakwepa, na wengine huamini kwamba kuwa karibu na watoto ni kuwadekeza na wanaweza kukuaibisha mbele za watu. Ikiwa familia itakuwa ni ya watoto watiifu tu kwa wazazi wao na hawana uhuru, basi hapo kuna utumwa.
UHURU BILA UTII NI WAZIMU: Pamoja na kuwa ni muhimu kwa watoto kupewa uhuru wa kujieleza na kutoa maoni yao katika masuala ya kifamilia na ya nje ya familia, kupendwa na kuoneshwa upendo hadharani na sirini, ni muhimu pia kukumbuka kuwa ni lazima pawepo na mipaka, na mipaka hiyo inawekwa na wote, wazazi lazima ndiyo wawe viongozi katika kuwashirikisha watoto juu ya mipaka yenyewe, mipaka iwe wazi kwa kila mmoja, ili kila inapotokea kuna mmoja anataka kuvuka mipaka akumbushwa na watoto wenziwe pasipo wazazi kutumia nguvu ya adhabu. Lakini utii ni njia tu ya kutimiza uamuzi
Pasipo kuwa na uhuru wenye mipaka ndipo aibu huja, ikiwa mtoto atawakosea adabu wazazi wake si matokeo ya kupendwa na kupewa uhuru, bali ni kwasababu nyumbani hapana mipaka ya uhuru . Watoto wapewe uhuru, wazazi wawe huru kwa watoto wao na uhuru huu uwe wenye mipaka ya wazi kwa wote.
Watoto wakiukosa upendo na uhuru nyumbani watautafuta nje, na ikiwa watafanikiwa kuupata huko madhara yake ni makubwa, kwa watoto wa kike ni mimba.
(Kwa habari ya watoto wa kiume nitajadili wakati mwingine)
Rafiki yako
Lazaro JP Kavageme
0787-654724/0769-085178
Social Plugin