KATAA UZOEFU

KATAA UZOEFU

clip_image002

Uzoefu ni kansa inayotafuna na kuathiri utendaji wa maelfu ya asasi za kiraia, mashirika ya dini na serikali. Lakini pia ugonjwa huu pia umeathiri watu wengi hasa vijana wasaka ajira kwenye nyanja mbalimbali za kitaaluma nchini. Kila mahali ni uzoefu, uzoefu, uzoefu!

Ajira zimekuwa ngumu kisa uzoefu, haupati ajira hadi uwe na uzoefu wa kazi unayoomba. Uzoefu umegeuka kuwa kigezo muhimu sana katika kupata ajira, kitu ambacho si sahihi, uzoefu hausomewi wala haufundishwi popote duniani. Hata hivyo neno lenyewe nadhani linakosewa namna linavyotumiwa ukilinganisha na mazingira yake; wanaposema uzoefu wanakuwa wanamaanisha muda fulani wa kufanya kazi, wanaposema wanahitaji mtu mwenye uzoefu wa miaka miwili na kuendelea wanamaanisha wanahitaji mtu aliyefanya kazi husika kwa miaka miwili na kuendelea, jambo ambalo ni kikwazo kikubwa kwa vijana wanaotoka vyuoni, wamepata wapi uzoefu.

Uzoefu ni kufanya kwa mazoea, mtu kufanya vile afanyavyo kila siku, hana jipya, hali ya mtu kufanya vile afanyavyo kila siku, hali hii hupelekea kupata matokeo yale yale na yeye kuendelea kuwa yuleyule. Namna hii huhatarisha ustawi wa familia, jamii na taifa.

Watu wanahofu kufanya mambo mapya kwa hofu ya kuchekwa na kuambiwa kuwa ‘unakuwa kama sio mzoefu wa kazi hii, hali hii kweli hutokea maeneo mengi ikiwa hayo mambo mapya hayataleta mafanikio kwa mara moja; na wakati mwingine watu wamehofu kupoteza nafasi zao za kazi.

Uzoefu ni ugonjwa unaoambukiza, kwasababu hata wakikupa kazi watakuambia ufanye chini ya mtu fulani ili upate uzoefu, na ni kweli watu wengi wameambukizwa/wamepewa uzoefu. Watu wengi waliokuwa mahiri wakati wa mwanzo wa kuanza kazi zao hizo baada ya muda fulani umahiri ule umeondoka na sasa wanafanya kwa uzoefu, hakuna tena ubunifu wa mambo wapya, maana wamewekwa chini ya mtu mzoefu.

Watu wanakwenda warsha na semina mbalimbali , wanapokea mambo mapya huko lakini wanaporudi makazini utaona mambo yanakwenda vilevile, semina wezeshi zimegeuka kuwa vijiwe vya kuongeza uzoefu na si maarifa mapya kwa ustawi wa taasisis husika.

Usikubali kuwa mzoefu, kukubali uzoefu ni kujifunga minyororo ya kukataa kufanya mambo mapya, punda ndiyo wanafanya mambo yaleyale kwakuwa hawana semina za kuwapa maarifa mapya na kuwafunza mbinu mpya kuboresha kazi zao.

Kataa kuitwa mzoefu, kataa kuajiri watu wenye uzoefu, kataa kuwa mzoefu, kataa kufanya kwa mazoea, kataa kuwa kama punda; uzoefu ni kukataa kupata maarifa mapya na kukataa kuyatumia ikiwa yatapatikana.

Rafiki yako

Lazaro JP Kavageme