Suala la kuoa na kuolewa ni suala muhimu na nyeti sana linalopaswa kufanywa kwa uangalifu na tahadhari kubwa kati ya watu wawili wanaooana, pamoja na familia zote mbili wanazotoka wanandoa. Ndoa huunganisha watu zaidi ya wawili japo ni muhimu na lazima hao wawili wanokubaliana kuishi pamoja wawepo; ndoa huunganisha kabila mbili na zaidi na koo mbili na zaidi kwa wakati mmoja na kwa tukio la mara moja tu, yaani kuoa ama kuolewa; ndoa huunganisha watu wa imani mbili na zaidi za kidini na imani tofauti.
Tangu zamani za mababu, suala la kuoa na kuolewa halikuchukuliwa kama jambo jepesi na rahisi hata kama walioa na kuolewa vijana wengi kwa kufuatana, bado halikuchukuliwa kama suala la kuzoeleka na kufanywa kwa mazoea. Kwasababu suala la kuoa na kuolewa kama tulivyoona hapo juu, lilikuwa ni jambo la pande mbili wanazotoka wanandoa, ilikuwa ni lazima familia hizi mbili wachunguzane kwanza ili kujiridhisha kuwa muoaji na muolewaji wanatoka katika familia ama ukoo wa watu wenye tabia nzuri, na hawana magonjwa ya kurithi.
Jambo la uchunguzi lilikuwa na mchakato mrefu na lilihusisha wazee wa pande zote mbili kwa mwanamume na mwanamke wanaooana, kufuatilia na kupata taarifa sahihi na kamili ndipo ndoa iruhusiwe kufungwa.
Ipo tofauti kidogo kati ya jamii za kale na za sasa linapokuja suala la kufuatilia tabia na hali ya magonjwa kwa familia na koo mbili wanazotoka wanandoa. Mara nyingi vijana wanaoingia kwenye ndoa wanapopeleka taarifa za uchumba kwa wazazi huwa wao tayari wameshakubaliana na hatua kubwa ya kukamilisha mahusiano ya kindoa tayari yanakuwa yameshafanyika kati yao wawili.
Leo hii hatujalli sana hali kabla, hali ya ukoo ama familia anapotoka muoaji ama muolewaji, kwa kiasi kikubwa hali hii inatokana na utawanyiko wa familia na koo, watoto kuwa mbali na wazazi kimasomo, kibiashara, na kazi. Hali hii haiwapi wazazi wengi kufuatilia hali ya familia ama ukoo mwingine anapotoka muaoji na muolewaji; ndio maana wazazi walio wengi wa sasa wanawasisitiza watoto wao angalau kuoa ama kuolewa na mtu wa kabila yake, imani yake, dini yake, na dhehebu lake.
Kwahiyo muoaji ama muolewaji anapopeleka taarifa za uchumba kwa wazazi, kwanza atakutana na swali hili ‘ni kabila gani huyo mwenzako’ ndipo yanafuata mengine kama ‘anafanya kazi / biashara gani, elimu yake, nk. Wengi wa vijana wakati wa sasa vigezo vyetu vikubwa si kabila, tabia za kifamilia, ama magonjwa, vigezo vyetu vikuu ni mvuto wa sura, elimu, kipato kwa maana ya kazi ama biashara, hii pengine inatokana na hali ya uchumi ya sasa kupanda, kwahiyo watu wanahitaji kusaidiana kifedha.
Hayo yote ni sawa, vigezo vyote vya kikale na vya kisasa vya kupata mume na mke ni sawa kabisa. Mimi ninataka nikuongeze kitu kinachotawala juu ya vigezo vyote hivyo, jambo hili ni “THAMANI YAKO”, kwamba oa ama olewa na mtu atakayeongeza thamani ya maisha yako, bila kujali anatoka ukoo gani, kabila gani, elimu yake, kazi yake, biashara yake, nk.
Watu husema kukosea mtu wa kuoa ama kuolewa ni kosa lisilosahihishika. Kila mtu ana haki ya kufurahia maisha yake, unapokuwa hauna fuaraha katika maisha yako, hauwezi kuona sababu ama kusudi la kuishi kwako. Kwakuwa suala la kuoa na kuolewa ni suala la hali ya wanandoa kuishi hivyo hadi kifo, ni muhimu sasa mtu kuchagua mtu atakayemuonesha thamani yake na kuiongeza, na hivyo kukufanya uwe mtu unayefurahia maisha yako kila siku.
Mungu ametuumba tukiwa na thamani kubwa sana, kila mtu jinsi alivyo ni hazina, ni mgodi unaotembea. Watu wengi hatuijui thamani yetu kwakuwa tumekosa watu wa kutuonesha thamani yetu na kisha kuiongeza thamani hiyo; thamani huongezwa huwa haikai katika hali hiyo hiyo wakati wote. Kama ilivyo kwenye sarafu ya nchi, nguvu ya sarafu ni thamani yake.
Utafanyaje?
Tafuta mtu atakayeipenda kazi yako, biashara yako, kilimo, nk, atakayekuwa radhi kufanya nawe ikiwezekana, atakayekutia moyo, atakayekuwa tayari kukuvumilia ukikwama, lakini pia atakayekusaidia kupata njia ya kutokea unapokwama, atakaye kusaidia kuweka akiba ya mapato yako, atakayekupongeza unapofanya vizuri.
Kwa namna hii utafurahia kila kitu chako. Wataalamu wa saikolojia wanasema kwamba mtu yeyote mwenye furaha huifanya kazi yake kikamilifu, na yeyote mweye kuifanya kazi yake kikamilifu huongeza thamani ya kazi yake, na yeyote mwenye kuiongeza thamani ya kazi yake, kazi yake humuongeza yeye thamani.
Kwa waliooa na kuolewa tayari tumia fomula hiyo hapo juu kuimarisha ndoa yako, kinachothaminiwa humlipa mwenye kukithamini, unapoongeza thamani ya mwenzako na wewe thamani yako inaongezeka. Katika mazingira haya ndipo huja ule msemo maarufu wa “kwanini Mungu hakukuleta mapema” ama “ulikuwa wapi zamani ?”
Ndoa nyingi zinavujika kwakuwa hakuna anayetia bidii kuongeza thamani ya mwenzake.
Hakuna mtu atakuonesha thamani yako kama hatafaidika moja kwa moja na thamani yako, mwenye kufaidika na thamani yako ni wewe mwenyewe kwanza, ndipo mkeo ama mumeo, halafu wanakuja watoto wenu, wazazi, na ndugu wengine.
Rafiki yako,
Lazaro JP Kavageme.
Social Plugin