UMASKINI WA WATOTO



UMASKINI WA WATOTO


Umaskini sio kitu cha lazima katika jumla nzima ya maisha ya mwanadamu, ni hali ya ukosefu wa mahitaji ya msingi katika maisha ya mwanadamu kwa wakati, kwa mfano mlo kamili, miundo mbinu ya maji safi na salama, mavazi, na miundombinu ya habari na mawasiliano. Umaskini ni duru na hali ya kunaswa; umaskini wenyewe una matawi manne, umaskini Kiroho, Kiuchumi, Kimwili, na Kijamii.

o   Kiroho; umaskini kiroho ni hali ya kukosa uhusiano sahihi na Mungu, na kukosa kuwa na njia ya uhakika kuishinda dhambi na kutokuwa na tumaini la uhakika kupata uzima wa milele.

o   Kiuchumi; umaskini kiuchumi ni ahali ya kukosa njia endelevu ya kujipatia mahitaji ya msingi ya maisha.

o   Kimwili; umaskini kimwili ni hali ya mwili ya kuwa katika dhiki, kuishi ama kuwepo katika mazingira yasiyo rafiki kwa afya ya mwili, kuugua magonjwa yanayoepukika, na hata kifo.

o   Kijamii; umaskini kijamii ni hali ya mtu kukubali mazingira duni na kujiona ya kwamba hana jinsi ya kuyabadili mazingira hayo na kuyatumia kuboresha maisha yake. 


Umaskini wa Watoto na vyanzo vyake:
Vipo vyanzo mbalimbali vya umaskini wa Watoto. Mapambano dhidi ya umaskini na jitihada za kuwatoa Watoto kwenye umaskini uliokithiri vinahitaji uelewa sahihi na mkamilifu wa vyanzo vya umaskini huo, japo vyanzo vyenyewe baadhi yake ni vigumu kudhaniwa ama kubainika.


  • Uzalishaji usiowiana na idadi ya walaji:
Kulingana na viwango vya uzalishaji, inaonekana kuwa katika nchi nyingi watu wanofanya kazi za kujenga ni asilimia ndogo sana ukilinganisha na walaji. Tena kasi ya kukua kwa uchumi ni ya chini ukilinganisha na kasi ya ongezeko la watu.  Katika nchi kama Tanzania ambapo 51% yao ni Watoto na vijana chini ya miaka 18, inaonekana kwamba wanaofanya kazi kuzalisha ni wachache lakini watu wote wanakula hicho hicho kinachozalishwa na hao wachache. Bado wanawake ndio hufanya kazi za uzalishaji kwa kiasi kikubwa  kwa kilimo cha jembe la mkono na bila kufuata kanuni za kilimo bora, zisizoleta uzalishaji unaohitajika kwa idadi ya Watoto. Hali hii inaendeleza umaskini. 

  • Matumizi mabaya ya mali, hasa fedha na mazao ya chakula:
Angalia! Watu walio wegi katika umaskini huwa na kasumba ya kutapanya fedha ama mazao waliyoyapata kwa wingi, ulevi na kuoa wanawake zaidi. Hali hii yamkini hutokana na kukosa uelewa wa kupanga vizuri kutumia vema mazao ama fedha zao; watu huwa na mtazamo wa msimu badala ya kuwa na mtazamo wa muda mrefu, kwa hiyo watu huchukulia kuwa vitu walivyo navyo ni vya msimu husika. Hata misemo ya Kiswahili “ponda mali kufa kwaja”, vunja mifupa angali meno yapo” nk

  • Uchumi mkubwa:
Mara nyingi mifumo ya kiuchumi inawapuuza Watoto kabisa, ukuaji wa uchumi unaweza kuongeza ugumu kwa mtu aliye katika umaskini. “Mpangilio wa uchumi katika miaka ya 1990, ulimaanisha kuwa Watoto walihitaji kwa haraka sana sehemu yao katika mafanikio ya Ulimwengu kwa kuwa wao ndio wenye uwezekano mdogo kabisa kunufaika na mafanikio”. {Kofi Annan; katibu wa zamani Umoja wa Mataifa}.

  • Uchangiaji wa gharama:
  Kuchangia gharama za msingi kama vile afya na elimu zina athali kwa vile zinagusa kwa nguvu zaidi ngazi ya familia na hivy okuzidisah ugumu zaidi wa watu waishio katika umaskini.

  • Uchumi wa mpito:
Lakini pia mabadiliko ya hali ya maisha kutokana na mabadiliko ya sera na mfumo, huenda yakafika akiwa yamechelewa na kukuta uwezekano wa Watoto kuondokana na umaskini umekwisha kupita.

  • Ubinafsishaji:
September 2002, Shirika la kuhudumia Watoto la SAVE THE CHILIDREN FUND, lilieleza kuwa kule kujihusisha kwa sekta binafsi katika kutoa huduma za msingi, kuna uwezekano wa kuwa na matokeo mabaya dhidi ya usawa na katika kupambambana na umaskini wa Watoto na kutimiza haki zao. Pia kutokana na ubinafsishaji na muelekeo wa kupanua secta binafsi, watumishi wengi wenye sifa na mafunzo yanayostahili walitoka kwenye secta ya umma, madhara yalikuwa ni kudorora kwa secta hiyo, huku Watoto walio katika umaskini wakiathiriwa zaidi.



  • Siasa na utawala:
Mazingira ya kisiasa na utawala yana uhusiano muhimu wa ustawi na maendeleo ya Watoto. Mazingira ya siasa na utawala yenye utulivu, amani, na mshikamano huruhusu huduma msingi za maisha kupatikana ipasavyo; mazingira ya siasa yenye vurugu na utengano  huleteleza fitina na Watoto ndio wenye kubeba ukatili wa madhara ya vita.

  • Mazingira:
Maumbile ya mazingira ambapo Watoto wanaiishi {kijiogafia ama hali ya hewa}, huchangia kuongeza ama kupunguza ukali wa maumivu ya umaskini. Watoto wanaozaliwa katika mazingira fulani wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata lishe duni, wakati wale wa mkoa mwingne  wanapata lishe stahiki kwazababu ya hali ya hewa na vipengele vingine vya mazingira.

  • VVU na UKIMWI:
Haipaswi kusahaulika kuwa afya, usalama na kupona kwa Watoto wote katika nchi zote zilizoathiliwa, yanakwamishwa na matokeo ya UKIMWI juu ya familia na jamii. Inakadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2020, Watoto milioni 106 chini ya umri wa miaka 15 kote duniani watakuwa wamepoteza mzazi mmoja ama wote wawili, huku Watoto milion 25 kuwa yatima kutokana VVU na UKIMWI: Barani Afrika, idadi ya yatima itaongezeka kufikia milioni 42, huku hapa Tanzania katika kila Watoto 8 chini ya miaka 15 mmoja atakuwa yatima, na zaidi ya nusu ya yatima wote watakuwa ni kwa sababu ya UKIMWI. Hali ya Watoto kuwa yatima inasababisha mazingira ya uhitaji mkubwa zaidi bila kuwa na msaada wa kufaa na wa uhakika: ugonjwa huu unapunguza uzalishaji katika kazi za kuajiriwa, biashara, na kilimo, na hivyo kudhoofisha mifumo ya kimaendeleo katika jamii: hii inaendeleza umaskini kwa Watoto.

Mwisho:

Maumivu ya umaskini humfanya mtu aliye katika umaskini ajione kwamba ameachwa bila msaada wowote na kwamba hakuna anayemjali wala mwenye uwezo wa kumsaidia, kwa maana hiyo umaskini ni kanusho la Upendo na Rehema za Mwenyezi Mungu kwa maskini.

Vyanzo vya umaskini wa watoto, kama tulivyoona hapo hapo juu ni vitu ama mazingira yanayoepukika. Tunaweza kukomesha umaskini huu ikiwa kila mmoja atachukua hatua kujiepusha na vitendo pamoja na kuepusha mazingira yanayopelekea hali zinazoleta na kuendeleza umaskini wa watoto.