Kuna kanuni moja inaitwa ‘the law of deterioration’ kwa
tafsiri isiyo rasmi ni kanuni ya uharibifu/mmomonyoko. Kanuni hii inaelezea
namna uharibifu mkubwa unavyoanza kwa hatua ndogondogo sana,
uharibifu/mmomonyoko huwa hautokei kwa mara moja, ama kwa ghafla.
Mmomonyoko sio lazima uwe wa udongo tu, kuna mmomonyoko wa
maadili pia, yote namna inavyoanza huwa si rahisi kuona ama kupima ukubwa wa
tatizo utakavyokuwa. Mmomonyoko wa udongo huanza kwa tabaka la juu la ardhi ya
eneo kuondolewa kidogo kidogo na ama maji, upepo, na wanyama wanaopita eneo
hilo mara kwa mara, na hatimaye korongo kubwa hutokea hapo ikiwa
hapakuchukuliwa hatua za kudhibiti visababishi vya mmomonyoko huo. Na gharama
za kuziba korongo huwa ni kubwa zaidi ya gharama za kuzuia viasababishi vya
mmomonyoko.
Kila kitu chenye mazalisho makubwa huanza kidogokidogo.
CHURA
Tuseme mfano wa chura, unapotaka kumpika chura, usimuweke
kwenye sufuria yenye maji yaliyokwisha chemka kabisa, ataruka na kukimbia,
lakini chura huyo huyo unapomuweka kwenye sufuria yenye maji ya baridi na kasha
kuitenga motoni chura huyo ataendelea kukaa humo huku akiendelea kujitahidi
kuzoea hali ya maji yanayochemka kidogo kidogo, mwisho maji yatachemka kiasi cha
chura kushindwa kustahimili joto la maji hayo, hapo ataamua kutoka nje ya
sufuria ya maji ya moto lakini bila mafanikio, hatafanikiwa kutoka humo
kwasababau hatakuwa na nguvu za kuruka nje kwakuwa amemaliz nguvu zake katika
kukabiliana na hali ya mabadiliko ya joto la maji yaliyokuwa yakichemka kidogo
kidogo, na kwa hivyo utakuwa umefauru kumpika chura akiwa hai.
Mabadiliko yeyote katika maisha ya mwanadamu bila kujali ni
mazuri ama mabaya huanza kidogo kidogo, taratibu taratibu, na mwisho
hukamilika.
Umaskini huanza kuja kidogo kidogo, na utajiri hali
kadharika, kufilisika nako pia, uzito wa mtu huanza kuongezeka kidogo kidogo na
kupungua uzito hali kadhalika. Kukua kiroho huanza kidogo kidogo, na kufa
kiroho huanza kidogo kidogo, umaarufu huanza kidogo kidogo, na huisha kidogo
kidogo, wawekezaji wakubwa wengi wao walianza kuwekeza kidogo kidogo, walikuwa
na mtaji mdogo.
MAFANIKIO/UTAJIRI
Kuna tatizo moja tu kwa watu wali wengi, wengi wetu
tunapenda mafanikio na utajiri, mafanikio ya haraka haraka, wengi wetu si
wavumilivu na tunakata tama mapema na kuzitelekeza ndoto zetu njiani kwakuwa
hatuwezi kuyasubiri mafanikio yanayokuja kidogo kidogo. Zipo kanuni za kufikia
utajiri, zote zinahusisha hatua ndogo ndogo na uvumilivu hatimaye kufikia
utajiri huo. Unaweza kufanikiwa sana kwenye biashara kwa kuanza na mtaji mdogo
ulionao.
Anza na hicho kidogo ulichonacho, kuwa na subira na
mvumilivu, mwishoni utapata kile kikubwa unachokihitaji, jambo lamsingi
usipoteze maono yako na dira ya kule uendako hata kama itakuchukua muda mrefu
kukamilika.
Usitafute njia za mkato kufikia matarajio na maono/ndoto
zako, zitakupeleka pabaya, watu wengi wameingia kwenye ushirikina kwa kutaka
kupita njia ya mkato kutimiza ndoto zao, wengi wamekuwa majambazi na mwishowe
kufa kifo kibaya kwa kutaka kupita mjia ya mkato kufikia ndoto zao. Mali yeyote
unayoipata kwa njia halali hukupa amani ya moyo, lakini mali ya udhalimu na
ushirikina huwa haina amani nawe.
Anza kidogo kidogo!
Social Plugin