Je ni kweli unaogopa KUTANGAZA NIA kwa kuhofia KUKATWA?
Kama kweli unaogopa kukatwa basi tangaza nia. Maneno haya mawili
"kutangaza nia, na kukatwa" yamekuwa ni maneno yaliyojipatia umaarufu
mkubwa sana kwa siku za hivi karibuni hapa nchini kwetu Tanzania, kwa
jinsi yanavyotumika na kuchukuliwa unaweza kudhani ni maneno mapya
kabisa pengine hata kwenye kamusi hayapo, yamekuwa ni kama maneno ya
msimu tu, lakini ukweli ni kuwa maneno haya yapo na tumekuwa tukiyatumia
mara nyingi tu kwenye shughuli zetu za kila siku, nyumbani na nje ya
nyumba zetu. wakati mwingine tumeyatumia moja kwa moja (directly)na
wakati mwingine si moja kwa moja (indirectly), unaweza usiseme kuwa
"ninatangaza nia" lakini kwa matendo yako na maneno yako fulani ukawa
unatangaza nia juu ya mambo kadha wa kadha unayotaka kuyafanikisha, nia
ni matamanio ama malengo; mara nyingi umetangaza nia pasipokutangaza
nia.
Kitu kikubwa kinachoyafanya maneno haya kuwa na msisimko wa aina yake ni
harakati na mchakato wa uchaguzi wa mambo ya kisiasa tunaoupitia muda
huu nchini mwetu.
Dhamira yangu si kujadili mambo ya harakati hizi za uchaguzi na
makandokando yake, nimedhamiria kuhamasisha mabadiliko ya maisha ya mtu
mmoja mmoja, kwa kutumia maneno haya maarufu na kwa wakati huu maarufu.
Nitaka nikwambie kwamba, usipotangaza nia ya kutumia muda wako vizuri
kubadilisha maisha yako, basi maisha haya yatakukata. Inatia huzuni sana
kuona kuwa wapo watu wanaishi maisha haya pasipokuwa na malengo
mahususi kwa kila dakika na saa inayopita, hawaujutii muda wanaoupoteza
kwa kukaa na kupiga porojo juu ya watia na wanaokatwa kwenye michakato
ya kisiasa, na ndiyo hao wanaotegemea wanasiasa wanaokatana wawaletee
maisha bora, kutwa ni kulaumu viongozi na serikali, wanashinda vijiweni
kusimuliana maisha ya watu wengine(majungu), wanapoteza muda mwingi
kwenye mitandao ya kijamii kufuatilia maisha ya wasanii wa bongofleva na
wa bongo muvi, wanatumia muda mwingi kupakua na kuposti picha na vitu
vingine vingi visivyokuwa na tija kwenye maisha yao, wanatumia muda
mwingi kufuatilia na kulike picha za watu wasiowafahamu, na wanatumia
muda mwingi kwenye TV.
Na kibaya zaidi wanatumia fedha kidogo wanayoipata kununua vitu wasivyo
vihitaji ili tu kujionesha kuwa nao wanajua matumizi. Wananunua vitu
kwakuwa ndiyo fasheni, ama kwakuwa jirani na fulani amenunua.
Ndugu yangu, fedha hiyo na muda huo hautarudi kamwe saa ikipita imepita,
na siku hali kadhalika, tumia huo muda kusoma kitabu kitakacholetea
tofauti chanya kwenye maisha yako angalau hata ukurasa mmoja tu kila
siku, na fanyia kazi hicho utakachojifunza, sikiliza CD zenye mafundisho
kuhusu kazi, biashara ama kitu chochote kinachoweza kukuletea
mabadiliko kwa kuboresha kazi ama hicho unachokifanya kukupatia mkate wa
kila siku; badala kukaa kijiweni na watu unaolingana nao mawazo tafuta
marafiki wapya wanaokuzidi hatua fulani maishani jifunze kutoka kwao,
itakubadilisha sana kimaisha, usiwaonee gere na kuanza kuzusha maneno
dhidi yao.
Wewe ni kiongozi na mtawala wa maisha yako, usiache vitu na watu watawale na kuongoza maisha yako.
Tangaza nia ya kutumia muda wako vizuri, na kuishi maisha ambayo
hujayazoea. Tangaza nia juu ya matumizi ya simu yako, juu ya marafiki
zako, juu ya vipindi unavyofuatilia kwenye TV yako.
Maisha hayatakukata ukichukua hatua hii ya KUTANGAZA NIA bali usipochukua hatua hii uwe na uhakika UTAKATWA!
Social Plugin