𝗦𝗵𝗮𝗺𝗯𝘂𝗹𝗶𝗼 𝗗𝗵𝗶𝗱𝗶 𝗬𝗮 𝗠𝗲𝘇𝗮 𝗬𝗮 𝗕𝘄𝗮𝗻𝗮


Ukristo umetokea kwenye dini ya Uyahudi (Judaism). Mara ya kwanza ulionekana ni kama kikundi ndani ya dini kubwa ya Uyahudi mfano wa Mafarisayo, Masadukayo, na Waesene. Walitumia kitabu kimoja, waliwarejea manabii walewale, walimtaja Mungu yuleyule – Yehova, walishiriki sikukuu nyingi kwa kufanana…. Na waliabudu siku moja kwenye jengo moja liitwalo SINAGOGI! Wayahudi walipata kibali na upendeleo kutoka kwa watawala, dola ya Rumi. Hivyo hawakutaka kuharibu mahusiano yao na watawala kwa sababu kwa kufanya hivyo wangejiingiza matatani na kujivutia mateso. Ili kujinasua kutoka kwenye hali ya kufananishwa na wakristo, watu wa dini ya kiyahudi waliamua kujipendekeza kwa watawala kwa kuwasema vibaya wakristo na ibada zao. Walianza kuishambulia ibada ya Meza ya Bwana. 

Waliwashitaki wakristo kwa watawala ya kwamba kila wakutanapo hula mwili na kunywa damu ya Yesu. Kwa hiyo ni dini ya watu wanaokula nyama na kunywa damu ya mtu – ni dini ya wauaji! Pili, waliwashitaki ya kwamba ni watu wanaoitana “kaka na dada” au kwa lugha ya zama hizi “wapendwa”. Sasa kwa kuwa wao (wakristo) walikuwa ni ndugu, maana yake walionekana na kutafsiriwa kutojali ndugu zao wengine na familia zao. Kwenye utamaduni wa Rumi (Kimsingi hata sasa kwenye nchi ya Italia na Hispania) familia ni kitu kinachokumbatiwa kwa thamani sana kuliko kitu kingine chochote. Yeyote anayekuja kuvuruga mpangilio huu wa kijamii huchukuliwa kama adui.

Hii ilikuwa ni kabla ya mfalme Theodosius wa dola ya Roma kutoa amri iliyoitwa 'amri ya Thesalonike', ambayo ilifanya Ukristo (wa kinikea) kuwa dini rasmi ya milki ya Roma, mnamo mwaka 380 BK.

Tunaposhiriki Meza ya Bwana tukumbuke watangulizi wetu walilipa gharama ya maisha yao kuiimarisha.