Mzuka ni nini?



MZUKA
Mzuka ni mzimu ni pepo ama jini. Ni pepo anaevalia sura ya mtu fulani aliyekufa na tena aliyekuwa na aliyekuwa akiheshimiwa na familia au ukoo, pepo hili huja ili kuleta ujumbe fulani na usio wa kawaida kwa watu wao. Mzuka huenda kwa watu wa jamii yake yaani watu wanaomfahamu mzuka na wanaotumainia nguvu za giza (uchawi)
Mzuka huletwa na wanajamii wake kwa kufanywa ibada maalumu na huondolewa pia kwa ibada maalumu, ibada hii huitwa tambiko, tambiko ni ibada ya kichawi, japo si kila tambiko hufanywa kwa lengo la kumleta mzuka, matambiko mengine hufanywa tu pasipo kuwa na lengo la kuleta mzuka (kuzukisha), mengine hufanywa ili kuondoa mikosi kwenye jamii, ukoo, au kabila husika, kuita mvua, kinga dhidi ya adui, nakadhalika. Ibada hii hufanywa makaburini ama nyumbani wakati wa usiku wa manane.
Tambiko huongozwa na kiongozi wa jamii/familia, ama ukoo. Ni lazima awe ni mtu anayezifahamu mila za jamii husika. Tambiko huambatana na sadaka, ni lazima wanafamilia watoe sadaka kwaajili ya ibada husika.
Ibada za kichawi si jambo jipya na wala si jambo la kizamani, ibada hizi zimekuwepo tangu wakati wa agano la kale (ki biblia) kabla ya kuja kwa Kristo, na zimeendelea hadi leo kwa baadhi ya watu, familia, koo, na kabila
Sijulizi katika biblia inamtaja mtu mmoja aliyekuwa mfalme wa taifa la Israeli, Sauli, 1Samweli 28:3-20, mlame Sauli alikwenda kwa mwanamke mchawi ili amzukishie mzuka wa nabii Samweli ili umtabirie ikiwa atapata ushindi vitani dhidi ya adui zake Wafilisti ama la. Kilichozungumza na mfalme Sauli hakuwa Samweli bali lilikuwa ni pepo lililovalia sura ya Samweli japo sauti na maneno yake vinasikikika ni kama mtumishi wa Mungu anayenena. Mzuka wa Samweli si Samweli, mzuka wa Samweli haukuwa Samweli!
Biblia inatuambia kuwa wafu hawana ufahamu wa jambo lolote katika ulimwengu huu, Mhubiri 9:5-6. Mtu anapokufa hawezi kurudia tena hali ya umbile la kidunia, mwili hubakia katika hali ya kuoza kaburini na roho yake ama iende kuzimu ama paradiso kutegemeana na mtu alikufa katika hali ya dhambi ama utakatifu.
Katika kitabu cha Ufunuo 14:13 Neno lipo wazi kabisa kuwa Mungu huwa hatendi kinyume na Neno lake, ikiwa anataka watu wapumzike baada kupitia tabu nyingi wakati wa uhai wao, ya nini awaruhusu tena warudi duniani kuzungumza na mtu, familia, ukoo, ama kabila fulani.
Roho za watu waliokufa pasipo kujali mahali zilipo kati ya Paradiso na kuzimu, ama walikuwa manabii, wachungaji, nk, hawana ruhusa ya kurudi tena ulimwenguni, Luka 16:19-31. Mungu hawezi kuwatumia tena kama wajumbe wake kuleta habari yeyote kwa mtu yeyote hapa duniani, bila kujali ni habari ya matumaini ama hukumu. Mungu akitaka kutuma wajumbe duniani kwa watu wake anao malaika mbinguni na anao watakatifu wake hapa duniani na si mizuka/mizimu.Mungu hakai katika ushirikina kwakuwa ushirikina ni matokeo ya nguvu za giza anazozitumia shetani kupotosha wanadamu; na tena Mungu amekataza ibada za kichawi kufanyika, Kumb 18:9-11, Isaya 8:19.
Ibada hizi Mungu anazichukia kwakuwa hazimpi yeye sifa na heshima anayoistahili, kukaza kuendelea na ibada hizi ni kumtumikia shetani, japo Mungu ametuachia uhuru wa kuchagua wa kumtumikia, ameagiza aabudiwe yeye tu, Kutoka 34:14, Luka 4:8.
Wengi wemetumbukia kwenye mtego pasipo wao kutambua, wanafanya ibada za matambiko kwa kudhani kuwa wanatimiza mila pendwa za familia, ukoo, ama makabila yao, wanamwabudu na kumtu kuza shetani pasipo ufahamu, wametingwa na kumezwa na kupofushwa na mila na tamaduni zao. Watu hawa wasipopata neema ya kufundishwa ukweli juu ya ubaya waufanyao, watapotea kabisa.
Jihadhari, shetani yupo kazini, hachoki kukutafuta, hakuogopi, na hana mpango wa kuchukua likizo.