
Halafu kuna wanaoshikilia kwamba Wakristo hata wasijihusishe kabisa na masuala ya kijamii au siasa! unapowaambia kuhusu mauaji na utoaji mimba au janga la ponografia wananung'unika tu na kudai kwamba hizi ni ishara za siku za mwisho! Kama kanisa tunachoweza kufanya ni kuomba tu", "kuhubiri Injili tu".
Mtazamo wa kwamba viongozi wa dini/Wakristo wasijihusishe Katika masuala ya Kisiasa, mtazamo huo mara nyingi huchochewa zaidi na uvivu, woga au ubinafsi na kukwepa wajibu. Kwa hakika wale watu wanaotumia visingizio hivyo vya juujuu ni kutotii amri zilizo wazi za Maandiko: "Mpende jirani yako kama nafsi yako." (Luka 10:27); “Nenda ukafanye vivyo hivyo” (Luka 10:37); Mithali 31:8 Fumbua kinywa chako kwa ajili yake aliye bubu; Uwatetee watu wote walioachwa peke yao;
Mithali 24:11 Uwaokoe wanaochukuliwa ili wauawe; Nao walio tayari kuchinjwa uwaopoe; Fanyeni mataifa yote kuwa wanafunzi” (Mt 28:19); "Basi mtu ye yote anayejua mema impasayo kufanya na asifanye, anafanya dhambi" (Yakobo 4:17)
Wale wanaoshikilia kwamba Wakristo hawapaswi kujihusisha na masuala ya kijamii au masuala ya kisiasa yanaonyesha kutojua kwao Biblia na historia ya Kanisa. Zaidi ya 70% ya Biblia inahusu masuala ya kijamii, na kisiasa. Ibrahimu alitumia nguvu za kijeshi kuwaokoa Lutu na familia yake kutoka wafalme wanne (Mwa. 14). Mungu alimwinua Yusufu kuwa kiongozi wa Misri (Mwanzo 41). Samweli, Nathani, Elisha, Isaya, Ezra - kwa kweli karibu manabii wote - walijihusisha sana na siasa kama washauri wa wafalme na kuwa na uvutano wa ki-Mungu katika mambo ya kitaifa. Musa, Eliya, Yeremia na Yohana Mbatizaji waliwakabili hadharani na kuwakemea watawala waovu.
Mfalme Daudi (mwanasiasa) alielezewa kuwa mtu anayeupendeza moyo wa Mungu” (Matendo 13:22).
Danieli na Mordekai wakawa mawaziri wakuu katika Babeli ya kipagani na kule Uajemi. Mungu alimwinua Debora na Malkia Esther kushika nyadhifa za uongozi wa kitaifa. Yoshua, Gideoni na Nehemia pia alishikilia nyadhifa za juu za kisiasa. Ezekieli 22:30 "Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu."
Mwaka 1077, Papa Gregory VII aliwahi kumtenga na kanisa Mfalme Henry IV, ilimbidi mfalme amtafute Papa ili atubu. Simulizi hiyo inaeleza kwamba Papa alimsubirisha mfalme kwa siku tatu ndipo akamruhusu amuone, haikua rahisi sababu mfalme alisubirishwa mahali penye baridi kali kwenye kitongoji cha Cannosa kilichopo milimani Kaskazini mwa Italia.
Mwalimu Nyerere JK, Katika kitabu chake 𝑩𝒊𝒏𝒂𝒅𝒂𝒎𝒖 𝒏𝒂 𝑴𝒂𝒆𝒏𝒅𝒆𝒍𝒆𝒐, anapotafakari kuhusu Kanisa na Maisha ya Watu, kwenye uk wa 101; Anasema hivi....
"Kwa hiyo, kila kitu kinachoshusha hadhi ya binadamu, asiishi kwa heshima na raha, lazima kishambuliwe na Kanisa na wale wanaolitumikia. Maana kwa kweli, hakuna utakatifu wo wote katika umaskini wa kulazimishwa, na ingawa mitaa michafu ya maskini yaweza ikazaa watakatifu, hatuwezi kudumisha mitaa michafu ya maskini ili izae watakatifu.
Mtu ye yote aliyevunjwa moyo kwa kulazimishwa kuishi katika hali ya unyonge, hana faida na nafsi yake, familia yake, wala taifa lake. Inawezekana ana faida kwa Mwenyezi Mungu; lakini hilo ni Mungu anayelijua.
Kanisa halina budi liwasaidie watu kuyagomea maisha yao ya dhiki; lazima liwasaidie kufanya hivyo haraka iwezekanavyo. Lakini lililo muhimu zaidi ni hili. Lazima idhihirike kwamba Kanisa linashambulia wazi wazi mtu au kikundi cho chote kinachosaidia kudumisha unyonge huo wa mwili na roho, bila ya kujali misukosuko inayoweza kutokea, kwa Kanisa au kwa wafuasi wake. Na po pote inapowezekana, na kwa hali yo yote inayowezekana, ni wajibu wa Kanisa kushirikiana na watu katika mipango kamili ya kujenga maisha yao ya siku zijazo katika msingi wa haki na usawa. Ni wajibu wa Kanisa kushiriki kwa vitendo katika kupanga, kuanzisha, na kuendeleza mabadiliko yaliyo ya lazima kwa binadamu, na ambayo lazima yatakuja, tutake tusitake.
Ni kwa kufanya hivyo tu, ndipo Kanisa litakapoweza kutarajia kupunguza chuki na kudumisha imani yake ya upendo kwa watu wote. Upendo wa Kanisa lazima uonekane katika vitendo vyake vya kupinga maovu, na kuleta mema. Maana ikiwa Kanisa halipingi maonevu yaliyoko, basi kuendelea kuwapo kwa Kanisa, na dini yote ya Kikristo, kutaambatanishwa na kuendelea kwa dhuluma".
Viongozi wa dini na kanisa Kutokujihusisha na siasa na masuala ya kijamii si tu ni kupuuzia historia ya Kanisa, pia ni kupuuzia Neno la Mungu.
Social Plugin